November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMFD yakoshwa serikali kuwekeza kisasa sekta ya uvuvi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online, Mwanza

Taasisi ya Waandishi wa Habari wa Kuendeleza Shughuli za Bahari na Uvuvi Tanzania (TMFD) imeipongeza serikali kwa kufanya uwekezaji wa kisasa kwenye sekta ya uvuvi Tanzania.

Akitoa taarifa kwa umma Januari 31,2024 Mkurugenzi wa TMFD Edwin Soko, ameeleza kuwa ugawaji wa boti za kisasa na vizimba vya kufugia samaki kwa wavuvi wa Kanda ya Ziwa ni hatua inayoonesha nia ya utekelezaji wa vitendo kwa Serikali katika kufanya mageuzi ndani ya sekta ya uvuvi na kuchochea dhana ya uchumi wa buluu.

“Uamuzi wa Serikali wa kuzindua boti za kisasa 160 na kati ya hizo 55 zimewanufaisha wavuvi 989 wa Kanda ya Ziwa pia ugawaji wa vizimba vya kufugia Samaki 222 na kuwanufaisha wafugaji wa samaki wapatao 1,213 kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa (Mwanza, Kagera, Geita, Simiyu na Mara) hii ni hatua muhimu inayoleta mwelekeo chanya kwenye sekta ya uvuvi Tanzania,”ameeleza Soko.

Soko ameeleza kuwa TMFD pia inapongeza dhamira ya Serikali kwenye matamanio yake ya kurasimisha sekta ya uvuvi kutoka kwenye mtazamo wa shughuli za kujikimu na kuifanya kuwa biashara kwani maamuzi haya yatawasaidia vijana na wanawake ambao ni wengi nchini.

“TMFD inaamini kuwa, mchango wa sekta ya uvuvi wa 1.8 % kwenye pato la Taifa haulingani na ukubwa wa shughuli zinazofanywa kwenye sekta ya uvuvi, hivyo jitihada zinazofanywa na Serikali zitaongeza mchango wa sekta hiyo kiuchumi,”ameeleza Soko.

Hata hivyo ameeleza kuwa TMFD inatambua jitihada zinazofanywa na Rais Samia Hassan Suluhu na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega kwa matamanio yao ya kutaka kuiona sekta hiyo inafanya vizuri.

TMFD inaiomba Serikali kuweka ruzuku kwenye sekta ya uvuvi kama ilivyo kwenye sekta ya kilimo na pia kuweka miongozo ya kuwawezesha wavuvi kukopesheka kwenye taasisi za kifedha.