March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMDA kuwatembelea wakulima na wafugaji

*Lengo ni kuwapatia elimu sahihi juu ya matumizi ya dawa

Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),Kanda ya Ziwa Mashariki,wanaandaa mpango kazi wa kuwatembelea  mara kwa mara, wakulima,wafugaji na wavuvi katika maeneo yao,ili kuwapatia elimu sahihi juu ya matumizi ya dawa.

Hayo yameelezwa Agosti 8,2025 na Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki,Aggrey Muhabuki,wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao kwenye kilele cha maonesho ya sikukuu ya Wakulima Nane Nane kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yaliofanyika Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki,Aggrey Muhabuki,akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao kwenye kilele cha maonesho ya sikukuu ya Wakulima Nane Nane kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yaliofanyika Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Aggrey amesema,kupitia maonesho hayo TMDA,imepata fursa ya kuwaona wadau mbalimbali na kuwaeleza namna sahihi ya matumizi ya dawa,vifaa tiba na vitendanishi.

“Safari hii tumekuwa na maonesho makubwa na watu ni wengi na sisi tulijipanga vizuri,tumekuja wataalamu wengi na watu  wote waliokuwa kwenye banda letu tumeweza kuwahudumia kwa wakati,”amesema Aggrey.

Pia amesema,kupitia maonesho hayo wamepata fursa ya kukutana na wakulima,wafugaji na wavuvi na kuwaeleza namna mbalimbali ambazo wanaweza kufanya biashara zao kwa kutumia dawa sahihi pamoja na kuwaelimisha juu ya usugu wa vimelea na viuavijasumu pale ambapo vingetumika kwa wafugaji isivyo sahihi.

“Tumekuwa tukizunguka kwenye mabanda  na  kuchukua taarifa za wafugaji mbalimbali na maonesho haya yamekwenda vizuri,tumefurahi kwani tumepata fursa ya kuona wadau ambao wengi ni wakulima,wafugaji na wavuvi, hivyo tutakuwa na mpango kazi wa kuwatembelea mara kwa mara na kuwapatia elimu sahihi juu ya matumizi ya dawa,”amesema Aggrey.

Pia amesema,matumizi ya dawa za kunenepeshea mifugo zinaweza kuleta athari kwa jamii endapo matumizi ya dawa hizo yatatumika vibaya na kusababisha athari kwenye mazao ya mifugo kama nyama,maziwa  na mayai.

“Hatari hiyo inaweza kutokea endapo hawatachukua tahadhari ya kutumia mazao hayo kabla ya muda ambao unastahili kusubili baada ya kutumia dawa hizo,”.