March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA:Mvua za msimu wa vuli kuwa za wastani hadi chini ya wastani

Na  Isaack Zenda,Timesmajira

MAMLAKA  ya hali ya hewa nchini (TMA), imesema kuwa msimu wa mvua za vuli Oktoba hadi Disemba mwaka huu zinatarajiwa kuwa za Wastani hadi Chini ya Wastani katika maeneo mengi na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki.

Mvua  hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, 2025 katikamaeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na kaskazini mwa mkoa wa kigoma na kusambaa katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba 2025. Mvua zinatarajiwa kuisha mwezi Januari, 2026.

Akitangaza utabiri huo leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a wakati akiongea na waandishi wa habari ,alisema licha ya mvua hizo  kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu lakini  zinatarajiwa kuongezeka kidogo mwezi Desemba, 2025.

Amesema mbali na mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinazotarajiwa, vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa katika msimu huu wa Vuli. 

Alisema msimu wa mvua za Vuli ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. 

“Kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa katika kipindi chote cha msimu  unatarajiwa kuwa na mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani katika maeneo mengi ya pwani ya kaskazini,  nyanda za juu kaskazini mashariki, mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza na Shinyanga. 

“Hata  hivyo, mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya  Kagera, Geita na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma,Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza  na ya pili ya mwezi Oktoba, 2025 katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara  na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na kusambaa katika maeneo ya mikoa ya Simiyu na  Shinyanga katika wiki ya nne ya Oktoba, 2025,”amesema

Aidha Dkt.Chang’a alisema mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba 2025 katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini. Mvua za msimu wa Vuli, 2025 zinatarajiwa kuisha mwezi Januari, 2026 katika maeneo mengi.

Amesema katika msimu huo kuna uwezekano wa kuwepo kwa El Niño hafifu pamoja na mabadiliko ya joto katika Bahari ya Hindi, hali itakayochangia mwenendo wa mvua za msimu huu.

Dkt. Chang’a ametoa onyo kwa wananchi  licha ya mvua kutarajiwa kuwa za kiwango cha chini katika maeneo mengi, bado matukio ya hali mbaya ya hewa yakiwemo vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza hivyo wananchi wanapaswa kufuatilia taarifa za kila siku kutoka TMA.

Ametaja miongoni mwa athari zinazotarajiwa kwa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo na chakula ambapo ukame wa udongo, kushuka kwa tija ya mazao, uwezekano wa mafuriko, magonjwa ya mimea na wadudu waharibifu. Wakulima wanashauriwa kupanda kwa wakati, kutumia pembejeo sahihi na kupata ushauri wa maafisa ugani.

Vilevile amesema katika sekta ya mifugo na uvuvi, uhaba wa maji na malisho, magonjwa ya mifugo kama homa ya bonde la ufa na miguu na midomo, pamoja na changamoto kwenye mazalia ya samaki. Wafugaji na wavuvi wanatakiwa kuweka akiba ya maji na chakula cha mifugo.

“Katika utalii na wanyamapori, kuna hatari ya migogoro kati ya wanyama pori na jamii kutokana na uhaba wa maji na malisho. TMA imezitaka mamlaka husika kuboresha miundombinu kwenye mbuga na mapori ya akiba.

“Kwenye usafiri na miundombinu, fursa ya kutekeleza miradi kutokana na vipindi virefu visivyo na mvua, lakini ukaguzi wa mara kwa mara unasisitizwa ili kuepuka madhara ya ghafla ya mvua kubwa,”amesema.

Kwa upande wa sekta binafsi, uzalishaji viwandani na biashara unaweza kuathiriwa kutokana na upungufu wa malighafi za kilimo huku Taasisi za fedha zimeshauriwa kuandaa huduma mahsusi ili kusaidia wadau kujenga ustahimilivu.