April 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA yawataka wananchi kuzifanyia kazi taarifa inazotoa

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online – Mwanza

Katika kipindi hiki cha mvua, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi kuchukua tahadhari , kuzingatia na kuzifanyia kazi taarifa inazozitoa,kwani ni sahihi kwa zaidi ya asilimia 85.

Pia TMA,imezishauri mamlaka zinazohusika  kuhakikisha mifereji na mitaro inasafishwa wakati wote ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi pindi mvua zinaponyesha.Huku utupaji wa taka ovyo unaelezwa kuwa chanzo kikuu cha kuziba kwa mitaro, hivyo wananchi wametakiwa kuacha mara moja tabia hiyo.

Akizungumza katika kikao cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha wa 2024/25 cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Meneja wa TMA Kanda ya Ziwa Victoria Augustino Nduganda, amesema, Januari 3, 2025, Kaimu Mkurugenzi wa TMA, kupitia kikao rasmi, alitoa mwelekeo wa mvua za msimu wa masika kwa maeneo yote yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka, yakiwemo ya Kanda ya Ziwa Victoria.

 Kwa mujibu wa TMA, mvua hizi zilitarajiwa kuanza wiki ya kwanza hadi ya pili ya Machi na kumalizika wiki ya kwanza ya Mei.

Hata hivyo Nduganda,amesema tathimini ya mvua kufikia Aprili 11, 2025, inaonesha kuwa mvua zilianza rasmi Machi 7 kama ilivyotabiriwa na katika mwezi Aprili kumeshuhudiwa ongezeko la mvua kubwa katika maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa Victoria, ikiwemo Mwanza.

Pia amesema,TMA ilitoa tahadhari Aprili 8, 2025 kwa maeneo mengi ya Kanda hiyo, ambapo mvua kubwa iliripotiwa kusababisha adha kwenye daraja la Mkuyuni na stendi ya Nyegezi. Wananchi wanakumbushwa kufuatilia taarifa hizi kwa karibu ili kuepuka madhara kwani ni sahihi kama zinavyotolewa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Ummy Wayayu, amesema Halmashauri yao inafanya tathmini ya maeneo hatarishi na kuhakikisha mitaro inasafishwa mara kwa mara.

 “Tunaelekeza sehemu ya mapato kwenye usafi na kuzibua mitaro ili kuepuka mafuriko.Nawaomba Wananchi wanaoishi mabondeni kuchukua tahadhari, na wale wenye mitaro inayopita karibu na makazi yao wahakikishe mazingira yao ni salama,”amesema Ummy.

Pia amewaasa wazazi kutowaruhusu watoto kuzurura ovyo kipindi hiki cha mvua nyingi kwani huenda wakajikuta kwenye hatari ya kusombwa na  mafuriko au kupata magonjwa kutokana na kucheza kwenye madimbwi.

Diwani wa Kata ya Buswelu, Sarah Ng’hwani, amewataka wananchi kuwahi kurudi nyumbani na kuhakikisha watoto wao wanakuwa sehemu salama.huku akiwahimiza walimu kuhakikisha watoto hawaachiwi kwenda nyumbani wakati wa mvua huku kwa wale wadogo zaidi wawasiliane na wazazi wao ili wawafuate.

Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Buzuruga,  Manusura Lusigaliye, amesema wamekuwa wakishirikiana na wataalamu wa afya kutoa elimu ya usafi kwa wakazi ili wasimwage taka kwenye mitaro.

Amewataka pia wananchi kuwa waangalifu na kujulisha uongozi mara moja endapo kutatokea dharura yoyote ya mafuriko  au nyumba kudondoka kipindi hiki cha mvua ili waweze kuwasaidia na wasiebdelee kupata madhara zaidi.