November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA yatoa taarifa ya Klimatolojia hali ya hewa ya mwaka 2021

Na Penina Malundo,timesmajira,online

MAMLAKA  ya Hali ya Hewa Tanzania  (TMA) imetoa taarifa ya klimatolojia hali ya hewa kwa mwaka 2021 ambapo imeonyesha kuwa mwaka huo, ulikuwa na joto la juu ya wastani wa muda mrefu (1981-2010) kwa kiwango cha nyuzi joto 0.50C.

Akitoa  taarifa hiyo leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi, amesema kuwa mwaka 2021 ulikuwa na joto la juu ya wastani wa muda mrefu hali iliyoathiri afya za binadamu na wanyama, uzalishaji, usindikaji na uhifadhi wa vyakula.

Amesema  Mwezi Novemba 2021 ulivunja rekodi ya kuwa na joto kali zaidi ikilinganishwa na miezi ya Novemba ya miaka ya nyuma tangu mwaka 1970 huku mwezi Disemba umekuwa wa tatu kwa kurekodi joto kali zaidi kwa mwaka huo tangu mwaka 1970.

Aidha, ripoti hiyo imeeleza kuwa nchi ilikuwa na upungufu wa mvua katika maeneo mengi yanayopata mvua za misimu miwili (kanda ya ziwa, nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini), hasa wakati wa msimu wa mvua za Vuli, Oktoba-Disemba 2021.

“Kwa wastani, mwezi Novemba 2021 ulikuwa na mvua kidogo kuliko miezi yote inayopata mvua za vuli kwa mwaka na umeshika nafasi ya tatu miongoni mwa miezi mikavu ya Novemba iliyowahi kutokea tangu mwaka 1970,”amesema na kuongeza

“Kipindi cha ukavu cha muda mrefu kilitokea katika miezi ya Oktoba na Disemba 2021 na kusababisha athari kubwa kwa jamii na uchumi hasa jamii za wafugaji ambapo idadi kubwa ya mifugo ilikufa kwa kukosa malisho na maji katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Manyara na Pwani”. Amesema Dkt Kijazi.

Aidha Dkt.Kijazi amesema taarifa hiyo kwa ujumla imeeleza kuwa mwaka 2021 ulikuwa na matukio ya hali mbaya ya hewa, hususan mvua kubwa, mafuriko, vipindi virefu vya hali ya ukavu, upepo mkali na hali ya joto kali, ambavyo viliathiri maisha kwa kiasi kikubwa.

Alifafanua kwamba kutokana na mabadiliko ya tabianchi, matukio ya hali mbaya ya hewa yamekuwa yakiongezeka idadi (frequency) na nguvu (strength).

Katika hatua nyingine, Dkt. Kijazi alitoa taarifa ya tathimini ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa (IPCC WGII report) iliyotolewa na Jopo la Kiserikali la Tathmni ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) ikieleza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanayojumuisha kuongezeka kwa idadi na ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo ukame na mvua kubwa pamoja na ongezeko la joto ambalo linatarajiwa kufikia nyuzi joto 1.50C ifikapo mwaka 2040 endapo hatua za kupunguza uzalishaji wa gesi ukaa hazitachukuliwa hasa kwa nchi zinazozalisha gesi hiyo kwa wingi duniani.

“Mabadiliko haya yameendelea kusababisha athari na madhara makubwa zaidi kwa jamii, viumbe hai na mfumo mzima  wa ikolojia,”amesema na kuongeza

“Uwezo wa kuhimili changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa utakuwa mashakani zaidi endapo ongezeko la joto litazidi nyuzi joto 1.50C”. Alieleza Dkt. Kijazi wakati akiwasilisha masuala yaliyoainishwa katika taarifa ya Jopo hilo la Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi. Taarifa hiyo ya jopo la kisayansi inapatikana katika tovuti ya IPCC,”amesema