Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
MKURUGENZI wa Huduma za Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania(TMA),Dkt.Hamza Kabelwa amesema kuwa mamlaka hiyo imekamilisha kwa asilimia 90 utengenezaji wa mitambo ya rada mbili Mkoani Mbeya na Kigoma.
Mkurugenzi huyo amesema hayo jijini hapa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu na vipaumbele vya mamlaka ambapo amesema mwaka 2021/22, mamlaka hiyo ineendelea na utekelezaji wa mradi huo wa rada, vifaa na miundombinu ya hali ya hewa ambazo hatua mbalimbali zimefikiwa.
Amefafanua kuwa kwa sasa TMA ina rada tatu zilizopo katika Jiji la Dar es Salaam, Mwanza na Mtwara ambazo zinafanya kazi ya kukusanya data za hali ya hewa zinazoonesha uhalisi wa anga la Tanzania.
“Wahandisi na waendesha mitambo tayari wameshapatiwa mafunzo katika kiwanda nchini Marekani kuhusu kuzihudumia na kuzitumia rada hizo,”amesema Kabelwa.
Aidha,Dkt. Kabelwa ameeleza kuwa mamlaka hiyo katika mwaka huo 2021/22 imeendelea na utengenezaji wa rada mbili zitakazofungwa katika Kiwanja cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na Jijini Dodoma ambapo ufungaji huo umefikia asilimia 45.
Hata hivyo amesema kuwa mamlaka hiyo ilifungua barua za dhamana kwa ajili ya malipo ya asilimia 80 ya kutengeneza rada hizo.
“Kukamilika kwa rada hizi kutakamilisha mtandao wa rada nchini wa kuwa na idadi ya rada saba na rada hizi zina uwezo wa kuona zaidi ya kilometa za mkato 450 huku zikizunguka na kuona matone madogo sana ya mvua katika hali ya uhalisia ndani ya kilometa 250,
“Mitambo hii pia itasaidia katika kukusanya data za hali ya hewa zinazooonesha uhalisia wa anga la Tanzania,”amesema.
Vilevile amesema kuwa mamlaka hiyo imetekeleza kazi ya kufunga mitambo miwili ya kupima hali ha hewa inaojiendesha yenyewe inayohamishika ambayo inavipimio 100, seti tano za vifaa vya kutambua matukio ya radi, vifaa 15 vya kupima mgandamizo wa hali ya hewa, vifaa 25 vya kulima kasi ya kiasi cha joto na unyevunyevu, mitambo minne ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe na vifaa vya kupima mvua vinavyojiendesha venyewe.
“Mamlaka tayari imepokea kompyuta maalumu ambayo ipo katika hatua za ufungaji, vilevile imezindua mfumo mpya wa uangazi wa hali ya hewa ya anga juu katika vituo vya kupima hali ha yewa ya anga ya juu kilichopo Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA),”amesema.
Akizungumzia vipaumbele vya mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/23 amesema mamlaka imeweka mkakati wa kuendelea kutoa huduma ya hali ha hewa nchini kwa kupanua uwigo wa utoaji elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa hali ya hewa.
“Mamlaka inaendelea kukamilisha ukarabati wa majengo ya chuo cha hali ya hewa Kigoma, na ukarabati wa vituo vya hali ya hewa vinane vilivyopo Singida, Songwe, Dodoma, Tabora, Mpanda, Mahenge, Songea na Shinyanga,”amesema.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa