Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online.
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema itaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia majukwaa mbalimbali, kuhakikisha jamii inachukua tahadhari pindi tukio la mawimbi yajulikanayo kama Tsunami yanapotokea.
Mawimbi hayo ambayo ni makubwa na maji yanayofikia urefu wa mita 30 na kusafiri kwa kasi ya kufikia kilomita 950 kwa saa na tukio hilo, linaweza kutokana na tetemeko la ardhi chini ya bahari, maporomoko ya ardhi, milipuko ya volkano, milipuko ya nyuklia na kuanguka kwa vimondo baharini, ambavyo husababisha kuhamisha ghafla kiasi kikubwa cha maji ya bahari yaliyo na nguvu kubwa na kusafiri kwa kasi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam, kila ifikapo Novemba, 5 kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Tsunami Duniani hiyo ni kutokana na makubaliano ya mwaka 2015 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo ilikubalika kuwa ni siku ya kimataifa ya kutoa elimu ya Tsunami kwa jamii.
Taarifa hiyo imesema, maadhimisho ya mwaka huu yanaadhimishwa na kauli mbiu isemayo ‘Utayari kwa Wimbi la Tsunami’, kauli mbiu hiyo ni mahususi kuzingatiwa kwani kumekuwa na ongezeko la matetemeko ya ardhi chini ya Bahari ya Hindi.
Imetolea mfano tememeko lililotokea hivi karibuni Agosti 12 mwaka huu saa 2 usiku lenye ukubwa wa kipimo cha lita 5.9 katika eneo la Kusini Mashariki mwa Mkoa wa Pwani katika Bahari ya Hindi.
Taarifa hiyo imesema, matokeo hayo ya Tsunami kwa kawaida hutokea mara cheche na hutokea ghafla na madhara yake ni makubwa kuliko aina nyingine za majanga.
“Serikali za nchi za ukanda wa Bahari ya Hindi kupitia Kamisheni yake ya masuala ya bahari inayosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa (UNESCO), zimefanya kazi kubwa kujenga mfumo wa tahadhari ya Tsunami, unaohusisha upimaji na utoaji wa tahadhari,” imesomeka taarifa hiyo na kuongeza;
“Kwa upande wa Tanzania, TMA inashirikiana kikamilifu na Idara ya Uratibu Maafa (Ofisi ya Waziri Mkuu) katika kuhakikisha tahadhari ya Tsunami inatolewa ipasavyo na hatua stahiki zinachukuliwa ili kupunguza maafa”.
Taarifa hiyo imesema athari za Tsunami, isababisha upotevu wa maisha ya watu, uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu katika muda wa dakika chache kutokana na mafuriko katika ukanda wa Pwani.
Imesema katika kuhakikisha mfumo wa tahadhari unafanya kazi ipasavyo, kila mwaka Tanzania hujihusisha katika maandalizi ya kukabiliana na Tsunami kwa kushiriki katika mazoezi ya kupima uwezo wa miundombinu ya mawasiliano katika nchi za ukanda wa Bahari ya Hindi.
“Septemba 2018, Tanzania ilishiriki katika zoezi la kukabiliana na janga la Tsunami kwenye Bahari ya Hindi.
“Zoezi hilo lilishirikisha wadau wa nchi 24 zinazozunguka Bahari ya Hindi, zoezi hili hufanyika kila baada ya miaka miwili, hivyo kwa mwaka huu hapa nchini, lilifanyika Oktoba 20 na kuhusisha wadau kutoka taasisi na Mamlaka ya Mkoa wa Dar es salaam,” imesema.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi