Na Bakari Lulela ,Timesmajira
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limetangaza rasmi kuwa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) za mwaka 2024 zitafanyika Desemba 13, 2025, huku dirisha la maombi kwa wasanii likifunguliwa rasmi jana.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana , Katibu Mtendaji wa BASATA, Dk Kedmon Mapana, alisema tuzo za msimu huu zina vipengele 36 kukiwa hakuna mabadiliko yoyote sawa na msimu uliopita.
“Leo tunazindua rasmi mfumo wa maombi ya kushiriki Tuzo za Muziki Tanzania 2024. Wasanii wote wanaweza kuanza kuomba kushindania vipengele mbalimbali kupitia mfumo huu mpya ambao umeboreshwa zaidi,” alisema Dk Mapana.
Kwa mujibu wa Dk Mapana, vipengele hivyo vinagusa aina mbalimbali za muziki nchini, vikiwemo Bongo Flavor, Singeli, Hip-Hop, Taarab, Dansi, Dancehall, Reggae na Muziki wa Asili.
Kati ya hivyo, Bongo Flavor imepata nafasi nne: Wimbo Bora wa Bongo Flavor wa Mwaka, Msanii Bora wa Kike wa Bongo Flavor, Msanii Bora wa Kiume wa Bongo Flavor, na Mtayarishaji Bora wa Muziki wa Bongo Flavor.
Kwa upande wa Singeli, kutakuwa na Msanii Bora wa Singeli, Wimbo Bora wa Singeli, na DJ Bora wa Singeli, huku Hip-Hop ikishindaniwa katika vipengele vya Mtayarishaji Bora wa Hip-Hop, Wimbo Bora wa Hip-Hop, na Msanii Bora wa Hip-Hop.
Aidha, Taarabu itakuwa na Mtunzi Bora wa Muziki wa Taarabu, Mwimbaji Bora wa Taarabu, na Wimbo Bora wa Taarabu, wakati Muziki wa Dansi utashindaniwa katika Mwimbaji Bora wa Muziki wa Dansi, Wimbo Bora wa Muziki wa Dansi, na Bendi Bora ya Muziki wa Dansi.
Kwa upande wa Dancehall na Reggae, kila moja itakuwa na tuzo mbili, huku muziki wa Asili ukiwa na kipengele kimoja cha Msanii Bora wa Muziki wa Asili wa Mwaka.
Dk Mapana ameongeza kuwa lengo la tuzo hizo ni kuendelea kuhamasisha ubunifu, ushindani wa haki, na kuinua thamani ya kazi za wasanii wa Tanzania ndani na nje ya nchi.
“Tunataka tuzo hizi ziendelee kuwa jukwaa la heshima kwa wasanii wetu. Tunawahimiza wote kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hii kuonyesha ubora wa kazi zao,” amesisitiza.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi