Judith Ferdinand,Timesmajira,Online,Mwanza
Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS),kimeongoza mjadala wa wazi juu ya mchakato wa kupata Katiba Mpya Tanzania ambao umeshirikisha makundi mbalimbali ikiwemo wanasiasa,waandishi wa habari,wanafunzi wa vyuo,bodaboda na wananchi.
Katika mjadala huo uliofanyika jijini Mwanza Mei 25, mwaka huu makundi hayo yalipata fursa yakutoa mapendekezo mbalimbali ambayo wanatamani yaingizwe kwenye katiba mpya kwa ustawi wa taifa ikiwemo kuondolewa kwa nafasi za Ubunge wa vitimaalum.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mjadala huo Mchambuzi wa masuala ya Kisiasa Deus Kibamba,amesema “Natamani siku moja atokee Rais atakaye amua kwamba ana andaa kipindi cha mpito yeye mwenyewe atangaze kuwa mimi ni Rais wa mpito ambacho tutafunua na kufanya mageuzi makubwa ya kikatiba hapo ndipo tunaweza kupata Katiba Mpya,”.
Kibamba ameeleza kuwa mfumo wa vitimaalum umekuwa chanzo cha kero kubwa kwani vinalalamikiwa hata na wanawake wenyewe kwani vinaufanya Ubunge wa vitimaalum uwe na hadhi ndogo kuliko Ubunge wa majimbo(wa kuchaguliwa).
“Mfumo mpya wa Katiba Mpya utakao kuwa umepatikana kama hautaenda mbali na kilichopendekezwa na Watanzania utaondoa na kufuta kabisa vitimaalum kwani vimekuwa vikilalamikiwa sana,”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Jukwaa la Katiba Tanzania Dkt.Ananilea Nkya,ameeleza kuwa nafasi za Vitimaalum vya wanawake kwenye uongozi Bungeni na Halmashauri viliwekwa Kikatiba kwa mujibu Ibara ya 66(1)B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 iliofanyiwa marekebisho mwaka 2005.
“Inasema kwamba kutakuwa na idadi ya wanawake wa vitimaalum ambao itakuwa ni asilimia 30,hivyo viti sisi wanawake tulivipigania kweli na viliingia miaka ya 1980 na viliwekwa kwa muda kwani wakati ule wa miaka ya 1970 hadi 1980 wanawake walikuwa siyo wengi kwenye nafasi za uongozi,tafiti zinaonesha kuwa walikuwa wanaogopa kwa sababu mfumo uliokuwepo zamani uliwanyima wanawake kufanya kazi nje ya nyumbani,”ameeleza na kuongeza kuwa;
“Tangu kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, mpaka leo ni miaka 30 tumeona wanawake wengi wamekuwa viongozi katika ngazi mbalimbali ,wametumia vitimaalum lakini vimekuwa siyo tena vya muda vimeendelea kuwa vya kudumu ambacho sicho tulichotarajia,tulitarajia watu waone kuwa mwanamke anaweza kuwa Mbunge na akagombea,”.
Dkt.Ananilea ameeleza kuwa licha ya nafasi hiyo kuwepo kikatiba lakini kutokana na uzoefu walioupata kwa sasa wanawake wamekuwa wanavipata kwa mbinde kwa njia ya unyanyasaji huku wachache wanapata kwa njia ya halali na hawawezi kupata fursa sawa kama wa kuchaguliwa mfano nafasi ya Waziri Mkuu mwanamke wa vitimaalum hawezi kuipata kwa sababu inataka Mbunge aliye chaguliwa.
Hivyo ameeleza kuwa kupitia jukwaa hilo wanapendekeza kufutwa majimbo na wawakilishi wa wananchi bungeni(wabunge), watoke kwa kila Wilaya(Wilaya zigeuzwe majimbo), kwa kuzingatia jinsi ya mwanaume na mwanamke ambapo jimbo moja linawakilishwa na watu wawili.
“Tunapendekeza mfumo wa vitimaalum ufutwe, kuwe na taratibu za majimbo kwa wagombe,kwa sasa tuna Wilaya Tanzania nzima 138 hiyo kama kila jimbo litawakilishwa na mwanamke na mwanaume kutakuwa na Wabunge 276 ukitoa Bunge la leo ambalo lina Wabunge 393 tutakuwa tumepunguza wabunge wa ziada 117 hivyo kuokoa fedha za umma na kuwa na usawa,”.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu(SHIVYAWATA),Wilaya ya Ilemela Sylvester Nkumillah ameeleza kuwa watu wenye ulemavu ni kundi lililosahaulika hata kwenye uwakilishi wao kwaio Katiba Mpya tunaomba izungumzie kwa kina kwamba ninamna gani mtu mwenye ulemavu anapatikananje katika nafasi ya uwakilishi kuanzia ngazi ya wenyeviti wa mitaa mpaka wabunge.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Bodaboda Mkoa wa Mwanza Joseph Msabila ,ameeleza kuwa wanahitaji Katiba yenye utashi wa kijamii ambayo itajumuisha watu wote.
Mwenyekiti wa TLS Kanda ya Ziwa Steven Kitale,amesema mapendekezo yatasaidia kujenga msingi imara ya Katiba inayozingatia matakwa ya wananchi hivyo serikali na viongozi wazingatie ili kuleta uwajibikaji na kuwapunguzia mzigo wananchi.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi