March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TLP yaunga mkono hatua ya Rais Samia kuanzisha maridhiano ya kisiasa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar

MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour Party Taifa (TLP), Richard Lyimo, ameunga mkono hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan,kuanzisha maridhiano ya kisiasa.

Ambapo amesema ni uamuzi wenye busara unaolenga kurejesha utulivu na kuokoa maisha ya Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es-Salaam, Lyimo amesema matukio yaliyotokea katika siku za karibuni yameathiri wananchi wasiokuwa na hatia, hivyo hatua ya Rais kukubali kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ni mwanzo mzuri katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizojitokeza.

“Maridhiano ni njia muhimu kwa watu waliokosa kuelewana kutafuta suluhu. Namshukuru Rais kwa kukubali kufanya mazungumzo na wanasiasa ili kubaini kasoro na kuchukua hatua stahiki,” amesema.

Lyimo amesisitiza kuwa maandamano yaliyopangwa hayapaswi kuendelea wakati ambapo Rais tayari ameonesha utayari wa kusikiliza na kujadiliana na wadau wa kisiasa.

“Sisemi kuwa wanaoandamana wana makosa, lakini kama Rais mwenye mamlaka ya kurekebisha penye hitilafu amekubali maridhiano, kuendelea kukaidi ni kuwaacha Watanzania waendelee kupoteza maisha. Siasa zinahitaji watu hai, siyo machafuko,”amesema.

Sanjari na hayo amewaonya watanzania kuwa maandamano mara nyingi huathiri watu wasiokuwa na hatia, hivyo ni muhimu kusitishwa ili kuepusha madhara zaidi.

Amesema fursa ya maridhiano ipo wazi na inaweza kujadili hata suala la maandamano endapo pande zote zitakaa pamoja mezani.

“Nawaomba wanasiasa na waandamanaji tusitishe vurugu na mawazo. Tuketi na Rais, tumsikilize, tujadiliane ili tusiumize Watanzania. Mimi naunga mkono maridhiano na naninapongeza kwa hatua hii,” amesema

Aidha, Lyimo ametoa wito kwa vyama vyote vya siasa kushiriki kikamilifu katika mchakato huo kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo alitoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na wale waliopata hasara ya mali kufuatia vurugu zilizojitokeza katika kipindi cha uchaguzi mkuu.