Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Geita
MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Nchini imeendelea kutoa msukumo mkubwa katika kuhamasisha uwekezaji nchini, kwa kutangaza fursa mpya zinazopatikana katika maeneo maalum ya kiuchumi, hasa katika Kanda ya Ziwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la TISEZA leo septemba 24,2025 kwenye maonyesho ya Teknolojia ya Madini , Ofisa Uwekezaji Mkuu wa TISEZA Kanda ya Ziwa, Erastus Malai, amesema kuwa mamlaka hiyo ipo mkoani humo kutangaza fursa za kipekee za uwekezaji, hususan katika sekta ya madini ndani ya eneo maalum la Buzwagi.
Malai amesema eneo hilo lina jumla ya hekari 1,333 ambazo zimetengwa rasmi kwa ajili ya shughuli za uchenjuaji wa madini.
Amesisitiza kuwa miundombinu yote muhimu kwa uwekezaji tayari ipo, ikiwemo majengo ya awali, barabara, ofisi, na ukaribu wa uwanja wa ndege huku akisema, mwekezaji hatalazimika kugharamia miundombinu hiyo, bali atahitaji kuwekeza moja kwa moja kwenye uzalishaji kama vile viwanda vya kuchakata madini.
Aidha,Malai amesema kuwa serikali iko tayari kutoa vivutio mbalimbali vya uwekezaji, ikiwemo vya kodi na visivyo vya kodi, kwa wawekezaji watakaowekeza katika eneo hilo maalum la Buzwagi.
Mbali na sekta ya madini, TISEZA pia imeeleza kuwa inahamasisha uwekezaji katika sekta nyingine muhimu zinazochangia uchumi wa Kanda ya Ziwa. Sekta hizo ni pamoja na kilimo, uvuvi, utalii, ujenzi wa majengo ya biashara, na ufugaji.
Kwa mujibu wa Malai, TISEZA imetenga maeneo mengine ya kiuchumi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa ajili ya uwekezaji wa sekta tofauti huku akiyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Nala mkoani Dodoma hekari 607 kwa ajili ya viwanda na huduma,Kwara, Kibaha mkoani Pwani hekari 100 na Bagamoyo hekari 151.
Amesisitiza kuwa maeneo haya yamelengwa kwa uwekezaji katika viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba, uundwaji wa magari na boti, bidhaa za ngozi, nguo, makazi, pamoja na vifaa vya matumizi ya majumbani.
“Hii ni bidhaa mpya kwetu sisi,” amesema Malai, “kwani ndio mara ya kwanza tunazindua maeneo haya rasmi kwa matumizi ya uwekezaji maalum kwa sekta mbalimbali.”
Ametumia nafasi hiyo kutoa wito wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kufika na kuchangamkia fursa hizi, hasa katika eneo la Buzwagi, ambapo serikali imeshawekeza miundombinu yote muhimu.
Aidha, mamlaka hiyo inawahimiza wafanyabiashara na wawekezaji kujitokeza pia katika sekta nyingine ambazo zina mchango mkubwa katika uchumi wa Kanda ya Ziwa.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina