December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TIRA Kanda ya Ziwa kuendelea kuelimisha wananchi umuhimu wa bima

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Kanda ya Ziwa, imeeleza kuwa inaelekeza nguvu katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa bima kwani takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 15 ya Watanzania ndio wenye uelewa kuhusu bima huku sekta hiyo ikiwa na mchango mdogo katika pato la taifa.

Sekta ya bima kitaifa inachangia pato la taifa asilimia 1.99 kwa takwimu za mwaka 2022 takribani asilimia mbili huku kati ya hizo mchango wa Kanda ya Ziwa ni asilimia 0.084.

Hayo yameelezwa Juni 21,2024 na Meneja wa TIRA,Kanda ya Ziwa, Richard Toyota wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari na Mawakili jijini Mwanza ili wafahamu huduma za bima ikiwa ni muendelezo wa mamlaka hiyo kutoa mafunzo na elimu kwa wadau mbalimbali.

Toyota ameeleza kuwa serikali imewapa malengo na maelekezo kuwa ifikapo mwaka 2030 angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe na uelewa wa bima huku sekta hiyo ikichangia asilimia 5 kwenye pato la taifa.

“Ukiangalia mchango wa sekta ya bima kwa Kanda ya Ziwa bado upo chini hatujafika hata asilimia 0.1, kitu ambacho tunaona tunahaja zaidi ya kupeleka elimu kwa ukaribu kwa wananchi,”.

Hata hivyo ameeleza kuwa katika asilimia hizo mchango mkubwa wa bima unatoka kwenye bima za magari ambao ni wa lazima kwani sheria imeelekeza kuwa huwezi kutumia chombo cha moto bila ya kuwa na bima,wanatamani Watanzania wengi wanunue bima zisizokuwa za lazima ikiwemo za maisha,ajali,afya.

“Kama kitaifa mchango utafikia asilimia tano basi Kanda ya Ziwa tutakuwa tumepiga hatua zaidi hivyo wakaona kukutana na waandishi wa habari pamoja na Mawakili ili waweze kutumika kama jukwaa la kupeleka elimu zaidi kwa wananchi juu ya umuhimu wa bima,”.

Mwanasheria Mwandamizi wa TIRA Kanda ya Ziwa, Wakili Aderickson Njunwa,amesema waandishi wa habari na mawakili wanayo nafasi kubwa ya kuelimisha wananchi kuhusu huduma za bima ili kupata haki za madai,malalamiko na migogoro inayohusu bima.

“Waandishi wa Habari tunaamini mkipata taarifa sahihi mtaifikia jamii kwa urahisi na elimu hiyo ya bima itakuwa sahihi, kwa kutambua hilo ndiyo maana tumekutana ili tukae pamoja,tupeane elimu ili mfahamu TIRA inafanya nini katika jamii,”amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Bima la Taifa (NIC),Kanda ya Ziwa, Stella Marwa amesema kuna aina tatu za bima ya kilimo (bima mseto,hali ya hewa na maeneo maalum),zinakatwa ili kuwakinga wakulima na wafugaji wanufaike na mazao yao pamoja na mifugo yao.

Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza (MPC), Edwin Soko amesema waandishi wa habari wawe mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu bima.

“MPC kwa kushirikiana na TIRA tunaweza kuanzisha tuzo za waandishi bora za bima ili kuhamasisha zaidi uandishi wa habari hizo,”amesema Soko.