Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetoa wito kwa wadhamini mbalimbali kuwaunga mkono wadau na waandaaji wa mashindano ya sanaa na urembo lakini pia kuwashika mkono vijana wenye vipaji ili kuhakikisha ndoto zao zinatimia.
Hayo ameyasema leo (Juni 9, 2022) Kaimu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA), Matiko Mniko wakati wa mkutano na waandishi wa Habari wa kutathimini kuhusu ushiriki wa Miss Tanzania Kanda ya Mashariki uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Katibu huyo amesema serikali imekuwa bega kwa bega katika kuhakikisha tasnia ya sanaa inakua kwa kuwaunga mkono wadau na wasanii kwa kutenga bajeti ya mfuko wa sanaa;
“Katika kutafuta warembo kunagharama kubwa zinatumika na mitaji inahitajika ndiyo maana tumeona katika bajeti ya serikali ya mwaka 2021-22 imeanzisha mfuko wa sanaa na utamaduni wenye malengo makubwa mawili mafunzo na mikopo hii ni baada ya kuona kwamba kuna haja kubwa ya kuwaunga mkono wasanii na wadau wa sanaa”
Aidha Mniko amesema Lengo la serikali ni kuhakikisha kwamba Taasisi mbalimbali ambazo zimejitolea kuunga mkono wasanii basi wanapata mikopo ambapo kwa mwaka huu 2022 kulitengwa bilioni 1.5 na mwaka 2023 bajeti imepitishwa ya Shilingi Bilioni 2.
Mniko amesema Lengo kuu la kuwepo na Baraza la Sanaa la Taifa BASATA ni kuitangaza sanaa, kukuza vipaji ili talanta ambazo vijana wamebarikiwa iwe sehemu ya kumpa ajira na kurudisha kwenye uchumi wa Taifa kuweza kulipa kodi na kuchangia pato la Taifa.
Kuhusu mipango ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Mniko amesema watakuwa na programu nyingi za mafunzo kwa wadau Kama makampuni na Taasisi zinazoendesha sanaa na wasanii wenyewe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tips Forum, Nancy Matta amesema katika shindano la Miss Tanzania Kanda ya Mashariki huko Morogoro lililofanyika tarehe 24/9 waliweza kutoa warembo watatu akiwemo Emanuela Slayo, Halima Ahmad Kopwe na Agnes Satura ambao walikwenda kuwawakilisha Kanda ya Mashariki kwenye mashindano ya Miss Tanzania;
“Tumeweza kumtoa mrembo Emanuel Slayo ambaye ameibuka kidedea katika kipengele Mrembo aliyekuwa anapendwa sana na watu (Miss Tanzania popularity), Mrembo Agnes Satura ambaye ndiye ameibuka miss Tanzania Top modal”
Aidha Nancy amesema wao kama Tips forum wanayo furaha kubwa sana kwa warembo hao kuweza kufanya vizuri sana kwenye mashindano ya Miss Tanzania akiwemo mrembo Halima Ahmad Kopwe ambaye ndiye miss Tanzania 2022 ambaye pia atakaeiwakilisha miss Tanzania kwenye miss world mwaka huu.
Pia Nancy amesema wakiwa pamoja na wadau wao wanayo furaha ya kufikia mafaniko hayo makubwa ambayo ni sehemu ya mpango mkakati wa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. samia Suluhu Hassan wa kuinua vipaji vya mabinti na nafasi ya mwanamke kwenye Jamii.
Mbali na hayo Nancy Amewashukuru BASATA kwa kuwa nao bega kwa bega kuhakikisha kwamba vipaji vya mabinti hao vinainuka na ndoto zao zinatimia.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito