Na Mwandishi Wetu Zanzibar , Zanzibar
TIMU za Mpira wa Kikapu kutoka visiwani Zanzibar zimetamba kufanya vema na kutwaa ubingwa wa mashindano ya CRDB Taifa Cup yatakayoanza kutimua vumbi Novemba 12 hadi 21 katika Viwanja vya Chinangali.
Katika mashindano hayo Zanzibar itawakilishwa na timu tatu mbili za wanaume kutoka Unguja na Pemba na moja ya wanawake kutoka Unguja.
Timu hizo leo asubuhi zimeondoka visiwani humo na msafara wa watu 45 na boti ya Azam Marine na baada ya kufika Dar es Salaam wamepanda mabasi kuelekea Dodoma tayari kwa mashindano hayo.
Msafara huo umeongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Zanzibar (BAZA) Rashid Hamza Khamis ambao unajumuisha wachezaji 36, makocha wanne, daktari wa timu, Matroni pamoja na viongozi watatu.
Kiongozi huyo amesema kuwa, timu zao zimejiandaa vizuri sana na wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri na kurudi na Ubingwa.
Lakini pia amewataka wadau mbalimbali wa mchezo huo kuendelea kusaidia timu zao kwani bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo bado zinawakabili.
Katika mashindano hayo, timu ya Unguja wanawake itatupa karata yake ya kwanza Novemba 13 dhidi ya CRDB wakati Unguja wanaume wakianza dhidi ya Arusha Novemba 14 huku Pemba akianza na Temeke.
Novemba 15 Iringa wanaume watawakaribisha Pemba wakati unguja wakivaana na Temeke
na siku inayofuata timu hizo zitakutana zenyewe kwa wenyewe na baada ya mchezo huo Pmba atakutana na Singida, Unguja atacheza dhidi ya Iringa wakati Unguja wanawake wakicheza dhidi ya Mbeya.
Hatua ya robo fainali itachezwa Novemba 19, nusu Fainali Novemba 20 huku mashindano hayo yakihitimishwa na mchezo wa fainali utakaochezwa Novemba 21.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania