Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mbio maarufu za Tigo Kili Half Marathon zikiwa ni mbio ambazo zipo ndani ya Kilimanjaro Marathon 2023 zimezinduliwa rasmi kimkoa katika viwanja vya Kibo Palace Hotel, Mjini Moshi kwa kushirikisha viongozi mbalimbali, wadhamini, Chama Cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro (KAAA), waandaaji wa mbio hizo na wadau mbalimbali.
Akizindua mbio hizo, Mkuu wa Wilaya wa Moshi, Mh. Abas Kayanda aliwapongeza wadhamnini na waandaaji wakiongozwa na Kilimanjaro Premium Lager 42km, Tigo-21km Grand Malt 5km na wadhamini wengine wa meza za maji kwa kazi nzuri na kusema wamezifanya mbio hizi ziwe maarufu zaidi na pia wameendelea kuutagaza Mkoa wake wa Kilimanjaro.
Mkuu huyo wa Wilaya aliipongeza kampuni ya Tigo kwa kutoa hamasa kwa watanzania na kuvumbia njia ya kujisajili kidijitali .
“Hii iwe changamoto kuwafanya watanzania wakimbie kwakasi zaidi ili washinde hata zawadi nyingine kubwa zinazotolewa na waandaaji.”
Alitoa wito kwa wafanya biashara kutumia fursa hii vizuri kwani wakati huu wa Kilimanjaro Marathon ndio muda wa kufanya biashara tofauti tofauti.
“Wenye mahoteli anzeni kufikiria kutoa ofa mbalimbali ili washiriki watenge muda zaidi wa kukimbia lakini pia kufanya utalii na wenye mabaa na makampuni mbalimbali mnaweza kuandaa promosheni ya wiki nzima kutangaza biashara zenu.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo alisema: Tigo inajivunia kuwa mdhamini mkuu wa Kilometa 21 yaani Tigo Kili Half Marathon kwa miaka minane (8) mfululizo ukizingatia umuhimu wa mbio hizi ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa mkoa wa Kilimanjaro pamoja na utalii hususan kanda hii ya Kaskazini kwa ujumla.
Kupitia mbio hizi, Kampuni ya Tigo imeendelea kuchangia katika kukuza utalii wa michezo (sports tourism) na vile vile kuchangia katika utunzaji wa mazingira kupitia mradi wa Tigo Green for Kili.
Kama wadhamini wakuu wa nusu marathon (21KM) tunayofuraha ya kushiriki katika kuzindua toleo la mbio hizi kwa mwaka huu wa 2023 kwa kushirikiana na Chama cha Riadha, Uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro ikiwemo vyombo vya ulinzi na Usalama, wadau wote wa utalii wa michezo/sport tourism na wadhamini wenzetu.
Kama tunavyofahamu usajili kwa ajili ya kushiriki kwenye mbio hizi ulishaanza tangu mwezi Octoba 2022 na bado unaendelea.
Tunapenda kuwakumbusha washiriki wote popote nchini nan je ya nchi kujisajili mapema kupitia Tigo Pesa kwa kupiga *150*01# kisha uchague Lipa Kwa Simu,halafu chagua tiketi ili kupata namba za ushiriki.
Mshiriki wa mbio hizi anatakiwa kuhifadhi ujumbe (SMS) na atatumia kama uthibitisho akiambatanisha na kitambulisho chake wakati wa kuchukua namba ya ushiriki katika vituo vilivyopo Dar es Salaam, Arusha na Moshi.
Katika mbio hizi, Tigo itatoa zawadi za kifedha zenye thamani ya Shilingi Milioni 12.5 kwa washindi 10 wa kwanza wa Tigo Kili Half Marathon (wanawake na wanaume).
Pia,washiriki 4,500 watakaomaliza Km 21 watapewa medali za heshima.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi