January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tigo yajivunia mafanikio, wazindua huduma ya eSIM

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kampuni inayoongoza katika kuhakikisha Watanzania wanafurahia maisha ya kidijitali, Tigo Tanzania, inajivunia kutangaza mafanikio ya hivi karibuni kupitia uzinduzi wa huduma ya eSIM.

Uzinduzi wa teknolojia ya eSIM ni hatua muhimu katika kutoa huduma bunifu kwa wateja wake.


Huduma ya eSIM inaahidi kuleta mageuzi ya kidijitali katika matumizi ya laini za simu na jinsi ambavyo wateja wanavyotumia simu zao za mkononi.

Tofauti na laini za simu za kawaida, eSIM hupachikwa moja kwa moja kwenye vifaa vinavyoendana na inaweza kuratibiwa kijijini na taarifa za mtandao.

Teknolojia hii ya kipekee inaondoa haja ya kutumia laini za simu na inawawezesha watumiaji kubadili mitandao au vifaa kwa urahisi.


Meneja Bidhaa,Eginga Mohamed kutoka Tigo Tanzania, ameelezea shauku yake kuhusu uzinduzi wa eSIM akisema, “Tigo Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika ubunifu wa kiteknolojia. Tunaamini katika kuendelea kuboresha na kutoa wateja huduma na bidhaa za ubunifu zaidi kuliko walivyotarajia. Hii ni hatua muhimu ambayo inawawezesha wateja wetu kuunganisha simu zao za mkononi kwa urahisi na usalama. Tunafuraha kuanza safari hii na kuwaletea wateja wetu huduma mpya ya matumizi ya kidijitali bila matatizo.”


“Kama sehemu ya uzinduzi wetu, Tigo Tanzania inafuraha kutangaza utaratibu rahisi wa kuwezesha eSIM, hivyo kurahisisha wateja wetu kuunganisha simu zao za mkononi. Kupitia ubunifu huu, watu wenye simu zinazoweza kutumia eSIM wanaweza kujiunga kwa urahisi na Mtandao wa Tigo, ambao unafungua mlango wa faida, vipengele, na matumizi mengi ambayo teknolojia ya eSIM inatoa. Aidha, uwezekano wa kuwa na eSIM zaidi ya moja kwenye kifaa kimoja kwa matumizi binafsi au ya biashara sasa ni jambo linalowezekana. Wateja wanaweza kuhakiki nambari zao mpya za kidijitali kwa urahisi kupitia nambari za QR,” amefafanua Eginga.


“Huduma ya e-SIM ya Tigo Tanzania inalenga kuimarisha dhamira ya kampuni ya kuvumbua na kuboresha uzoefu wa mawasiliano kwa wateja wake wote. Kama kampuni inayoongoza kwa ubunifu wa huduma za mawasiliano, eSIM ni sehemu tu ya mfululizo wa maendeleo makubwa,” amehitimisha Eginga.


Ili kufahamu iwapo simu yako inaweza kutumia huduma ya eSIM, mteja anaweza kupiga *#06# ili kuangalia nambari za EID. Kwa maelezo zaidi kuhusu eSIM ya Tigo Tanzania na vipengele vyake, tafadhali tembelea maduka yetu ya Tigo nchi nzima au piga 100.