January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tigo wakabidhi minara 42 kwa serikali ya mapinduzi Zanzibar

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema uzinduzi wa Minara ya mawasliano ya simu kwa kiasi kikubwa itaiwezesha Zanzibar kuingia katika Teknolojia ya Mawasiliano ya TEHAMA, ikiwa ni fursa muhimu kwa wananchi pamoja na kukua kwa sekta ya Uwezeshaji kiuchumi.

Dk. Mwinyi amesema hayo katika Ufunguzi wa minara 42 pamoja na vituo 11 vya TEHAMA huko Bwefuu, Mkoa Mjini Magharibi, iliojengwa kupitia fedha za Ruzuku za mfuko wa Mawasiliano kwa wote.

Alisema matumizi ya huduma za mawasiliano kwa sasa hayaepukiki kwa sababu mawasiliano yanagusa moja kwa moja maisha ya wananchi, ikiwemo walioko vijijini katika shughuli zao za kila siku.Akitolea Mfano, Dk. Mwinyi alisema matumizi ya TEHAMA yamekuwa yakiongezeka ikiwemo maeneo ya vijijini na kuchukua fursa kubwa za kiuchumi na hivyo kuongeza kipato cha wananchi.

“Nachukua nafasi hii kuupongeza Mfuko wa mawasiliano kwa wote kwa kushirikiana na Kampuni za Tigo/Zantel katika ujenzi wa Minara 42 na Vituo 11 vya TEHAMA hatua inayokwenda kufungua fursa muhimu za Uwekezaji na kiuchumi”, alisema.Aidha, Dk. Mwinyi aliwataka wakaazi wa maeneo hayo kuitunza miundombinu hiyo na uharibifu unaoweza kurudisha nyuma hatua kubwa ya maendeleo iliofikiwa.

Alisema miundombinu hiyo inahitaji kutunzwa na kuenziwa ili kuepuka uharibifu unaoweza kufanywa, hivyo akachukua fursa hiyo kuwataka Viongozi wa Shehiya kuhakikisha inalindwa.

Nae, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Dk. Khalid Salum Mohammed alisema uzinduzi wa minara hiyo ni sehemu ya ahadi ya kufikisha mawasiliano Vijini na kuondosha kabisa tofauti iliopo kati ya maeneo ya Miji na Vijiji.“Kinachofanyika leo ni kufikisha huduma za maendeleo kwa kasi kubwa ya kufikisha huduma za mawasiliano hadi Vijijini ili kuondosha tofauti na pengo la huduma hizo na kufika hadi Vijijini”, alisema.

Mapema,Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye aliupongeza Mfuko wa mawasiliano kwa wote ambayo ni Taasisi ya Muungano kwa kwa kazi kubwa ya kufikisha huduma za mawasiliano ya Internet kwa wanafunzi wa skuli 29 za Zanzibar pamoja na vifaa vyake, hatua ambayo itatoa nafasi nzuri kwao kufahamu matumizi ya TEHAMA na kuongeza ufaulu.

Alisema Mfuko wa mawasiliano kwa wote upo katika hatua za mwisho za kukamilisha Mradi wa kuunganisha mawasiliano ya huduma za Afya katika Hospitali ya Mnazimmoja na Hospitali neyngine, ikiwemo Muhimbili pamoja naTaasisi za magonjwa ya moyo ya Jakaya Kikwete ili kurahisissha huduma za mawasiliano ya Tiba na kuwafikia walengwa, mradi unaotarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Milioni 587.

Alisema ujenzi wa Minara hiyo na kituo cha TEHAMA ni sehemu ya miakkati ya kukuza Uchumi ili kwenda sambamba na Ilani ya Uchaguzi ya CCM , Dira ya Maendeleo pamoja na vipaumbele vya Serikali.Alisema kupitia mradi maalum wa mikakati , Mfuko wa mawasiliano kwa wote ulitoa jumla ya shilingi Bilioni 6.9 kwa ajili ya kusambaza huduma za mawasiliano kwa asilimia mia moja hadi Vijijini.

Aidha, alisema ujenzi wa Vituo 11 vya TEHAMA Unguja na Pemba ni hatua nyengine inayokwenda sambamba na azma ya kuwapatia wananchi huduma kwa wakati, ikiwemo kuratibu huduma za dharura na maafa.Alisema hatua hiyo ya uenzi wa Minara na kituo cha TEHAMA ni sehemu ya mikakati ya kukuza Uchumi ili kwenda sambamba na Ilani ya CCM.

Katika hatua nyengine, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote Justine Mashimba alisema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha mawasiliano yote yanafika Vijijini ili wananchi waweze kutumia fursa za kiuchumi.Alisema ujenzi wa minara 42 umetumia shilingi Milioni 6.9, hatua inayokwenda sambamba na mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuvutia Wawekezaji ili wawekeze katika miradi mikubwa ya kiuchumi.

Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mawasiliano na Miundombinu Suleiman Kakoso alizipongeza Serikali zote mbili kwa kuweka mikakati ya kuimarisha mundombinu ya mawasiliano, ambapo sasa yanakwenda kufungua huduma za Mawasiliano na TEHAMA hadi Vijijini.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akikabidhi tuzo kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa MIC Tanzania Kamal Okba wakati wa ufunguzi wa minara 42 pamoja na vituo 11 vya TEHAMA Bwefuu, Mkoa Mjini Magharibi, iliojengwa kupitia fedha za Ruzuku za mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF)