Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Bilinith Mahenge, ameipongeza kampuni ya Big Best kwa kuwekeza nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza, Dkt. Mahenge alisema, “Uamuzi wenu wa kuwekeza hapa ni wa muhimu sana. TIC itaendelea kuhakikisha kuwa mazingira ya uwekezaji yanaboreshwa ili kufanikisha mradi huu wa kimkakati.”
Ziara hiyo ni sehemu ya mpango wa Dkt. Mahenge kutembelea mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kutathmini utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uwekezaji.
Mikoa inayohusishwa na ziara hiyo ni Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, na Tabora. Lengo ni kufuatilia maendeleo ya miradi, kutambua changamoto zilizopo, na kuweka mikakati ya kuboresha utekelezaji wake kwa manufaa ya taifa na wananchi.
Kampuni ya Big Best inajihusisha na uzalishaji wa samaki aina ya Sato kwa kutumia teknolojia ya vizimba. Mradi huo unatarajiwa kuzalisha tani 900 hadi 1,200 za samaki kila mwezi ifikapo mwaka 2026.
Uwekezaji huo wenye thamani ya takriban dola milioni 30 za Kimarekani, unalenga kukabiliana na changamoto ya upungufu wa samaki nchini, kwa kuanza na kutosheleza mahitaji ya soko la ndani kabla ya kuanza kuuza nje ya nchi.
Dkt. Mahenge amepongeza manufaa ya mradi huo, yakiwemo ajira 400 za muda mfupi na za kudumu, uhamishaji wa teknolojia ya kisasa ya ufugaji wa samaki, pamoja na kuchangia kukuza uchumi wa mkoa wa Mwanza na taifa kwa ujumla.
Akizungumzia changamoto zinazokabili mradi huo, Dkt. Mahenge aliahidi kuwa TIC itashirikiana na taasisi mbalimbali kutafuta suluhisho la haraka.
“Ni jukumu letu kuhakikisha changamoto hizi zinashughulikiwa ili kuhakikisha miradi kama hii inafanikiwa na kunufaisha Watanzania,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa takwimu, mwaka 2024 Mwanza ilishika nafasi ya tano kitaifa kwa kuvutia uwekezaji, ikionesha kuwa mkoa huo unaendelea kuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji nchini.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini