December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TIC kuzindua vitendea kazi vyao

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kituo Cha Uwekezaji Tanzania TIC wanatarajia kuzindua vitendea kazi vyao ikiwemo mfumo wa huduma za wawekezaji kwa njia ya kielektroniki (Tanzania electronic investment Window )

Mfumo huo kwa awamu ya kwanza unaunganisha Taasisi 7 ikiwemo BRELA, TRA, TIC, Kamishna wa kazi, uhamiaji, NIDA na Ardhi

Hayo aliyasema Mkurugenzi wa Idara ya Uhamasishaji uwekezaji kutoka TIC, John Mnali wakati akizungumza na waandishi wa Habari Jana Jijini Dar es Salaam ambapo alisema uzinduzi huo utafanyika Septemba 16 mwaka huu kuanzia saa 12 jioni Katina hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Alisema Mfumo huo umetokana na kuunganishwa kwa mifumo ya Taasisi mbalimbali za serikali ambayo inashughulika na kutoa vibali na leseni mbalimbali kwa wawekezaji

“Kabla ya kuunganika ni kwamba Kila taasisi Ina mfumo wake lakini katika maboresho ambayo yamekua yakiendelea katika jitihada za kuwahudumia wawekezaji Taasisi hizi zimeunganisha mifumo yao ambayo inatumika katika kuwasajiki wawekezaji na kutoa vibali na leseni mbalimbali wanazozihitaji”

Mnali alisema kutokana na hivyo itakua imemrahisishia mwekezaji na hata muda wa kupata vibali na leseni mbalimbali kupitia mfumo huo utakua umepungua.

“Kwa awamu ya kwanza kupitia mfumo huo mwekezaji atakuwa anaingia kwenye mfumo mmoja ambapo atakapoanza usajili wa kampuni ataendelea kuomba vibali na leseni mbalimbali kupitia mfumo uleule mmoja”

“Zile taarifa za awali ambazo mwekezaji atakuwa amezitoa kuhusiana na jina au mmiliki wa kampuni n.k taarifa hizo pia zitaweza kupatikana na Taasisi zingine zote za serikali bila kulazimika Kila wakati kutoa taarifa Zile kwa wakati tofauti tofauti kama ilivyo bila ya kutumika mfumo”.

Mbali na hayo Mnali alisema katika mkutano huo pia watazindua muongozo utakaotumika kwa watu wanaotoa huduma kwa wawekezaji

“Hivi sasa baadhi ya wawekezaji wengine wapo nje ya nchi, wanaohitaji huduma hizi za kuweza kusaidiwa kuweza kupata vibali na leseni mbalimbali huwa wanafanyiwa na kampuni za ndani “

“Kwa kipindi kirefu hatukuwa na muongozo wa kuwaongoza wale watu wanaotoa huduma hii kwa wale wawekezaji ambao wanataka kufanya uwekezaji”

Kadhalika Mnali alisema watazindua kampeni maalum ya Uhamasishaji uwekezaji wa ndani na nje.

“Kuna juhudi mbalimbali zinaendelea za kuweza kuvutia wawekezaji nchini na katika juhudi hizo kwanza tunahamasisha wawekezaji wa ndani waweze kuanzisha miradi mbalimbali ya uwekezaji kwenye Sekta mbalimbali zilizopo nchini lakini pia tunahamasisha uwekezaji wa nje kuja nchini kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji”