March 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TIB yawekeza bil.630.3 kwenye miradi ukiwemo wa kupunguza njaa

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

BENKI ya Maendeleo(TIB)imesema imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 630.3 katika miradi ya maendeleo hadi kufikia Desemba 2024.

Ambapo kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 408.3 zipo kwenye mizania ya Benki,huku mifuko tisa inayosimamiwa na Benki ikichangia uwekezaji
wa Shilingi bilioni 222.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo Machi 20,2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Lilian Mbassy wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Benki hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo amesema uwekezaji huo ni wa miradi ya muda wa miaka 5-15 katika sekta
mbalimbali za maendeleo.

Mbassy ameeleza kuwa uwekezaji huo umegusa maeneo ya kipaumbele ya Serikali pamoja na malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambapo bil.162.7 zimewekezwa kuongeza usalama wa chakula na kupunguza njaa.

Huku bil. 4.3 zimewekezwa
kuboresha elimu kupitia miradi ya taasisi za elimu na Shilingi 22.4 bilioni zimewekezwa katika upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira kupitia miradi ya mamlaka za maji.

“Uwekezaji mwengine ni Shilingi 11.5 bilioni zimewekezwa katika nishati safi na nafuu kupitia mradi wa upanuzi wa nishati ya umeme vijijini (Tanzania Rural Electrification Expansion Programme-TREEP),na bil. 250.7  zimewekezwa katika ukuaji wa uchumi na ajira, ikihusisha sekta za utalii, viwanda, na usafirishaji na Shilingi 24.7 bilioni
zimewekezwa kuboresha miji na makazi,”amesema Mbassy.

Aidha Mkurugenzi huyo amesema kuwa kupitia uwekezaji huo zaidi ya ajira mpya 12,547 zimezalishwa kutokana na Benki kufadhili miradi ya muda wa kati na mrefu nchini.

Akizungumzia mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya Benki hiyo,Mbassy
amesema TIB kama benki ya maendeleo ni taasisi ya kisera ambayo ina jukumu la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa hususani kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo mwaka 2025,vipaumbele vyake vimejikita katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa ili kuongeza kasi ya maendeleo,pamoja na kutekeleza vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita.

Vilevile amesema kuwa Benki itaendelea kukuza mtaji wa Benki kwa kushirikiana na taasisi za fedha za kimataifa ili kupata mikopo ya riba nafuu kwaajili ya kufadhili miradi mikubwa ya
maendeleo yenye athari Chanya kwa jamii na uchumi.