Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Hamad Chande ameitaka Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kuhakikisha inaendeleza jitihada za kufanya tafiti ambazo zitasaidia kupatikana majawabu ya changamoto mbalimbali ambazo Taifa linakabiliana nazo.
Ameyasema hayo Desemba 2, 2022 Jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya Ishirini(20) ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi za Dar es Salaam na Mtwara ambapo ameongeza kuwa iende sambamba na kutoa mafunzo yanayowaandaa wahitimu wanaokidhi mahitaji ya soko kwa kuzingatia mapinduzi ya nne ya viwanda.
Aidha, ameipongeza kwa kuweza kuandaa na kuzindua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Kimataifa wa Usimamizi wa Biashara na Maendeleo ya Uchumi ambao ulifanyika tarehe Novemba 29,2022 Jijini Dar es Salaam.
“Utafiti ndio uhai wa maendeleo ya uchumi wa nchi yoyote duniani. Nawapongeza kwa kuanzisha jukwaa hili. Majukwaa ya namna hii yenye lengo la kuishauri Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kupitia tafiti mbalimbali; yawe endelevu”. amesema
Amesema ili kukabiliana na changamoto za usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma, mahitaji ya soko, ushindani na utandawazi; tunahitaji wataalamu wenye weledi, maarifa, umahiri na ubunifu.
“Nimefurahishwa sana na mikakati mnayopanga na jitihada mnazofanya katika eneo hili. Endeleeni kuzingatia kwa umakini suala la umahiri katika mitaala yenu ili tuendelee kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kuleta mabadiliko kiuchumi”. amesema Chande
Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania Prof. William Pallangyo amesema TIA imeendelea kutekeleza majukumu yake makuu ya kutoa mafunzo, kufanya utafiti na kutoa huduma ya ushauri wa kitaalam kwa kuongeza ufanisi.
Amesema tangu mahafali ya mwaka 2021, Taasisi imefanya maboresho mbalimbali katika utoaji mafunzo, utafiti, ushauri wa kitaalam, maendeleo ya watumishi, matumizi ya TEHAMA na miradi ya maendeleo inayojumuisha miundombinu ya kusomea na kufundishia.
amesema TIA imefanikiwa kwa mara ya kwanza kuanzisha kozi za Shahada ya Uzami zipatazo tanoambazo zimejikita katika maeneo ya uhasibu na fedha, ugavi, usimamizi wa biashara katika miradi, rasilimali watu na TEHAMA, pamoja na masoko na uhusiano wa umma.
Pamoja na hayo amesema Taasisi imejiunga na mfumo wa kupata taarifa kwa njia ya mtandao chini ya umoja wa vyuo vikuu na maktaba za tafiti (COTUL) yenye kanzi data za Ebscohost na Emerald na kanzi data nyingine zipatazo 19.
Hata hivyo ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kutoa shilingi Bilioni 7.8 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa jengo la Taaluma katika Kampasi ya Mwanza.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja