November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahasibu wapewa mafunzo utawala bora

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA,) pamoja na mameneja wa kampasi za taasisi hiyo kutoka mikoa sita nchini wamepewa mafunzo maalumu ya Utawala Bora yaliyotolewa na Taasisi ya Wakurugenzi (Institute of Directors.) kwa lengo la kuimarisha utendaji na sekta ya utawala.

Kufuatia mafunzo hayo, viongozi hao kila mmoja kwa nafasi yake wametakiwa kuwajibika ili kuyafikia malengo yaliyowekwa na Taasisi hiyo adhimu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania Dkt. Modest Assenga, amesema mafunzo hayo yamelenga kuimarisha maendeleo ya taasisi hiyo pamoja na kujenga maslahi bora kwa Serikali, Watanzania kwa kuzingatia ushirikiano na kutimiza wajibu kwa Bodi ya Ushauri ya Taasisi na Utawala.

Amesema katika mafunzo hayo watabadilishana uzoefu ili kuyafikia malengo ya Taasisi hiyo hasa kwa kusimamia rasilimali za taasisi pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali.

”Taasisi hii tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikitekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kutoa elimu, kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi na biashara pamoja na kutoa ushauri kuhusiana na masuala mbalimbali ya kiuchumi na biashara, hivyo kupitia mafunzo haya tunaamini tutaapigaa hatua zaidi na kuipeleka Taasisi yetu mbali zaidi,” amesema.

Kuhusiana na changamoto zinazoikumba Taasisi hiyo, Assenga amesema kuwa, licha ya kuwepo kwa taasissi za namna hiyo, TIA imejipanga kwa kutumia silaha ya kutoa kozi zitakazowawezesha wahitimu kujiajiri na sio kutegemea kuajiriwa moja kwa moja.

Muonekano wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) iliyoko Mkoa wa Singida

”TIA ina matawi mengi nchini na tumepanga katika kukaabiliana na ushindani na hiyo ni pamoja na kuendelea kusambaa kwa matawi ya Taasisi hii kote nchini,” amesema.

Kuhusiana na suala la wahasibu wengi kutokuwa waaminifu katika maeneo walioajiriwa, Assenga amesema taasisi hiyo imekuwa ikiwajenga wanafunzi kwa nidhamu ya hali ya juu katika usimamizi wa feddha na kusema kuwa ni nadra kusikia wahitimu wa Taasisi hiyo wakikutwa na hatia ya matukio ya ubadhilifu wa fedha katika maeneo wanayofanya kazi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA,) Said Chiguma amesema mafunzo hayo ya siku mbili yamefika wakati muafaka wakati Taasisi hiyo ikielekea kupata bodi mpya itakayoshirikiana na utawala ili kuyafikia malengo ya Taasisi pamoja na kubadilishana uzoefu na ujuzi.

Amesema mafunzo hayo yaliyowakutanisha na wakuu wa matawi sita ya TIA, viongozi wa utawala na bodi ya ushauri ni katika kufanikisha malengo yaliyowekwa na Taasisi hiyo na kusema kuwa wafanyakazi wategemee viongozi imara na wanafunzi wategemee kupokea mafunzo kwa haki na utaratibu uliowekwa pamoja na utatuzi wa changamoto zinazowakabili.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wakuu wa matawi ya taasisi hiyo kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Kigoma, Singida na Mtwara.