Na Penina Malundo ,Timesmajira
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umezindua mpango mkakati wa miaka mitano (2023-2027) unaotarajiwa kutumia kiasi cha sh.Bilion 46.1 katika utekelezaji wa majukumu ya utetezi wa haki za binadamu.
Mpango mkakati huo umezinduliwa rasmi juzi katika Hoteli Coral Beach jijini Dar es Salaam, na Afisa Program wa THRDC, Remmy Lema amesema mpango utajikita katika maeneo matatu muhimu, ambapo eneo la kwanza ni ulinzi na usalama kwa Watetezi wa Haki za Binadamu Nchini.
“THRDC inatarajia kuwajengea uwezo Watetezi wa Haki za Binadamu ili kuweza kukabiliana na changamoto za utetezi, pia katika eneo hilo mpango kazi unalenga kuongeza uchechemuzi wa kuwezesha mabadiliko ya sheria mbalimbali ambazo sio rafiki katika jitihada za kukuza na kulinda haki za binadamu nchini,”amesema na kuongeza
Aidha amesema eneo la pili ambalo limepewa kipaumbele zaidi katika mapango huo ni, Usimamizi na uratibu wa Wanachama pamoja na ushiriki wa jamii katika utetezi wa haki za binadamu, ambapo katika eneo hilo THRDC inakusudia kuwajengea uwezo wanachama, kuwawezesha kupata fursa mbalimbali za kuendeleza majukumu ya utetezi, kuwajengea mazingira rafiki ya kupata wadau wa kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ueledi na mafanikio, pia kuzijengea uwezo jamii katika masuala mbalimbali yanagusa utetezi wa haki za Binadamu.
Ametaja eneo la tatu katika mpango huo ni, Ukuzaji na uendelezaji wa taasisi, ambapo katika eneo hilo THRDC itakuwa na jukumu la utafutaji wa rasilimali pamoja na usimamizi pia kukuza ushirikiano wa kitaasisi na wadau wengine kwa kujenga uhusiano wenye tija na manufaa katika utekelezaji wa majukumu ya utetezi wa haki za Binadamu nchini.
Amesema mpango kazi huo unatarajiwa kutekelezwa kimkakati kwa awamu mbili (term) ambapo awamu ya kwanza inatarajiwa kuanza mwaka 2023-2024 huku awamu nyingine ikitarajiwa kufanyika 2025-2027 ikiwa lengo ni kuwezesha mpango kazi huo kufanyika kwa ufanisi na mafanikio kama ilivyokusudiwa.
Hata hivyo amesema THRDC, imeyajumuhisha baadhi ya mambo muhimu ambayo yalikuwa kwenye mpango mkakati uliomalizika, likiwemo suala la mkakati wa kuwezesha upatikanaji wa sheria inayotambua na kulinda watetezi wa haki za binadamu nchini, ambapo katika suala hilo mpango mkakati mpya utarajia kuongeza mazingira ya uchechemuzi ili kufanikisha suala hilo ambalo linatazamiwa kuongeza mazingira rafiki ya watetezi wa haki za binadamu nchini endapo likifanikiwa kwa wakati.
Amesema mpango mkakati huo unatarajiwa kuiendeleza ofisi mpya ya THRDC – Zanzibar ambayo imeanza kutekeleza majukumu yake hivi karibuni kwa kupanua wigo wa utetezi haki za binadamu Tanzania Zanzibar kwenye masuala mbalimbali ikiwemo uchechemuzi katika kuwezesha mabadiliko ya sheria zisizo rafiki kama ambavyo tayari jukumu hilo limeanza kufanyika siku chache mara baada ya ufunguzi wa tawi hilo ambalo kwa sasa lina wanachama zaidi ya 30.
More Stories
Mwabukusi akemea wanasiasa wanaotoa kauli za kibaguzi kuelekea uchaguzi mkuu
TAA yatakiwa kulipia mirabaha inayohusiana na matumizi ya muziki katika viwanja vya ndege nchini
Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini yafanya ziara ya kujifunza uongezaji thamani wa madini nchini Zambia