Na Penina Malundo,Timesmajira,Online
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeendesha semina elekezi kwa wanachama wapya wapatao 70 wa Mtandao huo ikiwa na lengo la kuwapitisha wanachama hao na kuweza kufahamu kazi za Mtandao pamoja na kufahamiana.
Akizungumza wakati wa Kufungua warsha hiyo leo,Mratibu wa THRDC,Onesmo Olengurumwa amesema mkutano huo ni wa siku mbili ambao unalenga kuwapitisha na kuwaelekeza wanachama hao wapya sera,misingi na mambo yanayoingoza THRDC .
Amesema THRDC kama kikundi hakina budi kuwa na sheria na kanuni zake hivyo semina hiyo ina lengo zuri la kuwapitisha wanachama hao na kuweza kufahamu kazi za Mtandao pamoja na kufahamiana.
“Semina hii ipo kwa malengo mazuri kabisa kwanza wewe mwenyewe tukufahamu lakini pia na wewe uufahamu mtandao na misingi yake, lengo ni kuwasaidia kufahamiana, mtandao unawasaidia kuwaleta pamoja, tuitumie ni fursa vizuri ,”amesema Olengurumwa huku akiwasisitiza wanachama hao kuendelea kufanya vizuri katika kazi za utetezi ili Mtandao uendelee kuonekana ukifanya vizuri nchini.
Aidha Olengurumwa amesisitiza kuwa ni lazima mtu awe mtetezi kweli wa haki za binadamu ili aendelee kuwa mwanachama wa THRDC.
“Msingi mkubwa na kigezo kikubwa cha kuwa mwanachama hapa ni kutetea haki ,ukiacha kutetea haki manake ni kuwa uanachama wako unaanza kuwa kwenye shida, unaanza kutushawishi uongozi uone kwamba ulikosea kukusajili kuwa mwanachama,”amesema
Pia amesema pamoja na kuwa wanachama hao wanafanya vizuri katika kazi za kiutetezi katika maeneo wanayofanyia kazi lakini kumekuwepo na changamoto ya utunzaji wa kumbukumbu ya kazi hizo na kuwataka wanachama wa THRDC kuhakikisha wanatunza kumbukumbu vizuri ikiwemo picha zenye ubora na kuzituma kazi zao kwa sekretariet ya mtandao ili ziweze kuwekwa kwenye tovuti.
“Jitahidini kuweka kumbukumbu vizuri na ndio maana tukaanzisha utaratibu na huu ni utaratibu wa lazima ukishakuwa mwanachama wetu kila mwaka utume taarifa ya kazi mnazozifanya na sio lazima usubiri mwaka uishe,”amesema
Ameongeza kuwa kama watetezi wa haki za binadamu wanapaswa kujitahidi kujinadi katika maeneo waliyojikita kufanyia kazi kwa kufanya jambo moja na sio kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na kuwataka wanachama kufanya kazi kwa kushirikiana ili waweze kufanikiwa.
“Wanachama wetu wako wengi na katika kila eneo unalofanyia kazi jitahidi kuwa na uelewa mpana wa mambo,usiwe mtetezi ambaye ukiulizwa kwanini isiwe hivi huna sababu za kisheria,kuelewa unachokitetea ni silaha mojawapo ya kukufanya uendelee na kazi yako” ameeleza Olengurumwa na kuwataka wanachama kufanya kazi zao za utetezi wa haki za binadamu kwa kuzingatia sheria na matakwa ya kikatiba.
Kwa upande wake Afisa Dawati la Wanachama THRDC, Joyce Eliezer ameendelea amewataka wanachama wa Mtandao kuhakikisha wanatunza kumbukumbu za kazi wanazozifanya ili kama mtandao uweze kutangaza kazi wanazozifanya.
More Stories
SACP Katabazi Elimu ya usafirishaji wa kemikali muhimu kwa watanzania
REA yajitosa kwenye nishati safi ya kupikia
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume