May 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

THRDC yatoa Jaketi za usalama kwa JOWUTA

Mwandishi wetu,TimesmajiraOnline,Dar

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binaadamu Tanzania(THRDC) umekabidhi jaketi za usalama kwa waandishi  wanachama wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania(JOWUTA) huku ikimuomba Rais Samia Suluhu kurejesha maridhiano ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Makabidhiano ya Jaketi hizo,yamefanyika Mei 2,2025 katika Hoteli ya Mbezi Garden, jijini Dar es Salaam ambapo wanahabari kutoka mikoa yote nchini walikuwa wakipatiwa mafunzo kuhusiana na uchaguzi mkuu yaliyoandaliwa na THRDC.

Mratibu wa Kitaifa wa THRDC ,Wakili Onesmo Ole Ngurumwa akizungumza katika makabidhiabo hayo, aliwataka wanahabari nchini kuyavaa katika harakati zao za kazi na hasa uchaguzi mkuu ili kutambulika na kujikinga na mashambulizi kama yakijitokeza.

Ole Ngurumwa alisema,Wanahabari ni miongoni mwa watetezi wa haki za binaadamu hivyo wanapaswa kulindwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“THRDC kwa kushirikiana na Taasisi za Wanahabari,JOWUTA,MISA-Tanzania,UTPC na MCT tutaendelea kushirikiana kuhakikisha mazingira ya kazi.ya wanahabari yanakuwa salama”alisema

Hata hivyo,aliwataka wanahabari kutumia Taaluma yao vizuri kusaidia jamii kufanya maamuzi sahihi hasa wakati huu wa uchaguzi.

“Binafsi ningependa kipindi hiki vyombo vya habari viongeze mijadala,habari na chambuzi kuhusiana na uchaguzi mkuu ili kuongeza uelewa kwa wananchi badala kutumia muda mrefu kujadili kamali,michezo na vituko vya wasanii”alisema

Ole Ngurumwa pia alitumia mafunzo hayo kumuomba Rais Samia Suluhu,kukubali uwepo wa maridhiano ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu.

“Tunamuomba sana Rais wetu,kurejesha maridhiano kinachoendelea sasa halina afya kwa taifa letu kuelekea uchaguzi mkuu”alisema

Ole Ngurumwa pia alieleza THRDC inalaani matukio ya ukiukwaji haki za binaadamu ikiwepo kuvamiwa Katibu Mkuu wa baraza la Maaskofu  padri Charles Kitime na kutekwa mwanaharakati mwanachama wa chadema Saidi Nyangali maarufu kwa jina la  Mdude.

Wakitoa mada katika mafunzo hayo mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba,Deusi Kibamba,Mwanahabari Jesse Kwayu,Mtendaji Mkuu wa UTPC Keneth Simbaya na Wakili Paul Kisabo, wote waliwataka.wanahabari kufanyakazi kwa kuzingatia maadili ili kulisaidia taifa

Kibamba alisema bado vyombo vya habari vingi havijatimiza wajibu kuelimisha jamii juu ya masuala muhimu kwa taifa ikiwepo Tanzania kuwa na uchaguzi Huru na Haki.

Wakili Kisabo aliwakumbusha wanahabari juu ya sheria mbalimbali na Kanuni za Uchaguzi ambazo hata hivyo zilionekana kuvibana vyombo vya habari.ikiwepo kuzuiwa kutangaza habari za wagombea ambao watazuiwa kufanyakampeni na kamati za maadili lakini pia kuzuiwa waangalizi wa uchaguzi kuzungumza na vyombo vya habari bila idhini ya tume

Akizungumza katika mafunzo hayo,Mwenyekiti wa JOWUTA ,Mussa Juma alisema kuna haja ya Taasisi za wanahabari kukutana na Tume huru ya uchaguzi ili kujadiliana juu ya kanuni za uchaguzi.

“Tumeona kuna vifungu kadhaa vya kanuni za uchaguzi vinaminya uhuru wa wanahabari kufanyakazi  na wanahabari wengi hawana uelewa”alisema.

Hata hivyo Juma ,alishukuru ushirikiano baina ya THRDC na JOWUTA ikiwepo kuandaa mafunzo ya kuripoti uchaguzi na masuala ya ulinzi na usalama kwa wanahabari katika uchaguzi na kuwapa jaketi.

“JOWUTA kwa kishirikiana na THRDC na shirikisho la wanahabari la kimataifa(IFJ)tumetoa mafunzo kwa wanahabari katika mikoa ya Morogoro,Dar es Salaam,Pwani,Mbeya,Iringa,Njombe,Arusha ,Kilimanjaro na Manyara na tunajipanga kuendelea na awamu ya pili”alisema

Juma aliomba Taasisi nyingine kujitokeza kushirikiana na JOWUTA yenye wanachama nchi nzima kutoa mafunzo kwa wanahabari ikiwepo ya matumizi sahihi ya akili mnemba(AI) kuelekea uchaguzi Mkuu.