Na Penina Malundo, timesmajira
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umesema kuwa bado kuna changamoto za utekelezaji wa kauli za Rais ambazo zinagusa masuala ya haki za binadamu.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Mratibu Kitaifa THRDC, Onesmo Olengurumwa wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa maelekezo mazuri juu ya masuala ya haki za binadamu lakini watendaji wake wanamuangusha kwa kushindwa kuyatekeleza.
Amesema Rais Samia amezungumza kwa nguvu zote kuhusu haki za wafungwa na watuhumiwa kwamba uchunguzi ufanyike kabla ya kukamatwa na kwamba wasikae siku nyingi rumande bila kwemda mahakamani, lakini jambo hilo limekuwa halitekelezwi.
Olengurumwa amesema kadiri muda unavyozidi kwenda nchi imeendelea kubaki kwenye mawazo na kauli, utendaji wa yale yanayoyazungumza kama Taifa kuanzia ngazi ya juu mpaka chini yanazidi kufifia.
“Mfano kauli ya Rais ilikuwa mfumo wa utoaji haki jinai usitumike kama njia ya kuwaumiza watanzania, kwahifadhi watu rumande kwa siku nyingi bila kuwapeleka katika vyombo vya utoaji haki, sasa kuna viongozi 24 ambao ni watetezi wa haki za binadamu huko Loliondo wanakwenda miezi minne wapo ndani uelekeo wa kesi yao haujulikani.
“Sasa hapo tunajiuliza maagizo yanatoka kwaajili ya kumsaidia nani, kama watanzania wale na wengine wapo ndani bila kupelekwa mahakamani, ni muhimu kwa watendaji na watu wengine wanaohusika kujitahidi kutekeleza maagizo ya Rais kwa mujibu wa taratibu za kisheria tulizonazo katika Taifa,” amesema Olengurumwa
Amesisitiza kuwa wametoa mifano ya Loliondo na Ngorongoro juu ya viongozi hao ambao licha ya maagizo ya Rais walipaswa kufikishwa katika vyombo vya sheria ili kama walihusika na makosa walioshutumiwa waweze kuhukumiwa na kama hawahusiki waachiwe huru lakini jambo hilo halijafanyika mpaka sasa.
More Stories
Tanzania ipo tayari kupokea wakuu wa nchi,mkutano wa nishati-Dkt.Kazungu
Chunya yafikiwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
HGWT yawarejesha kwao wasichana 88 waliokimbia ukeketaji