December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

The Desk &Chair foundation yawafariji watoto wenye migongo wazi,vichwa vikubwa

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

KITUO cha kulelea watoto wenye migongo wazi na vicwa vikubwa cha Nyumba ya Matumaini (Hope House),kimepokea msaada wa vifaa mbalimbali vya milioni 7,kutoka Taasisi ya The Desk & Chair Foundation .

Msaada huo ni pamoja na viti mwendo,mashuka,vifaa vya elimu na kilimo cha umwagiliaji wa matone,uliokabidhiwa kituoni hapo Mei 12,2024 kwa watoto na watumishi wa kituo hicho.

Akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa Taasisi hiyo,Dkt.Alhaji Sibtain Meghjee, amesema wametoa viti mwendo vitano,vyandarua 10,mashuka 40,vifaa saidizi vya walemavu 2,boksi tano za vifaa vya kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya matone.

Vifaa vingine ni boksi moja la sabuni za kuogea na miche ya kufulia pamoja na madaftari 100 na Counter books 10 kwa watoto wenye mgongo wazi na vichwa vikubwa wanaolelewa katika kituo cha Nyumba ya Matumaini Kitongo .

Kwa upande wake Meneja wa Kituo cha Nyumba ya Matumaini cha Kitongo ,Getrude Leizer amesema,msaada huo umesaidia kituo hicho kwa hatua kubwa huku akiwaomba wadau wengine wajitokeze kuwasaidia watoto hao ili watimize ndoto zao.

Pia ameishukuru taasisi hiyo kwa kuwaondolea adha na changamoto ya ukosefu wa maji baada ya kuunganishwa katika mtandao wa maji wa mradi mkubwa wa kisima cha Kitongosima.

“Tulikuwa na changamoto ya ukosefu wa majisafi na salama kwa watumishi wa kituo na watoto pia, maji ya matumizi ya kilimo cha umwagiliaji wa bustani ya mboga mboga na matunda,”amesema Laizer.

Kwa upande wake mlezi wa watoto wa kituo hicho,Rechal Kakaya amesema hawakuwa na maji safi na salama ya kunywa na matumizi mingine baada ya kuunganishwa katika mradi wa kisima sasa watoto watabadilisha mazingira ya shule.