September 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

The Desk &Chair Foundation yakabidhi miundombinu ya maji gereza la Butimba

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

TAASISI ya The Desk & Chair Foundation katika kuadhimisha siku ya Ashura, imefadhili matanki matano ya kuhifadhia maji safi na mabomba ya mita 300 yenye upana wa inchi 2 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya maji safi na salama katika Gereza Kuu la Butimba mkoani Mwanza .

Aidha taasisi hiyo hivi karibuni imechimba na kujenga kisima kirefu katika eneo la Gereza hilo la Butimba kitakachowahudumia watu takribani 3,000 kwa siku wakiwemo wafungwa, watumishi wa gereza na familia zao.

Kupatikana kwa huduma ya maji katika gereza hilo kutawaondolea watumishi, wafungwa na mahabusu changamoto ya uhaba wa maji kwa matumizi mbalimbali.

Taasisi hiyo imewashukuru wafadhili wote kwa kuwezesha miradi hiyo ya kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kiuchumi.

Katika hatua nyingine waumini wa dhehebu la Shia Ithna Sheria jijini Mwanza, wameadhimisha Siku ya Ashura kwa maandamano ikiwa ni kukimbikizi ya kifo cha Imamu Hussein Ibn Ali aliyeuawa katika ardhi ya Karbala.

Imamu Hussein ambaye ni Mjukuu wa Mtume Muhhamad S.A.W.anatajwa kuwa Imamu wa kwanza wa dini ya Kiislamu ya dhehebu la Shia, aliuawa pamoja na wengi wa watu wa familia yake.

Taasisi ya The Desk & Chair Foundation kila mwaka imekuwa ikiadhimisha siku ya kifo cha Imamu Hussein kwa kupanda miti ama kuchimba kisima cha maji kwa ajili ya kusaidia jamii ikiwa ni kumbukumbu ya namna Imamu huyo alivyozingirwa na watesi wake na kunyimwa maji ya kunywa.

Pia waumini wa dhehebu hilo wamekuwa wakimkumbuka Imamu Hussein kwa kufanya mambo mbalimbali ya kijamii kama kupanda miti na kuchimba visima vya maji.