Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Bunda
Wakazi wa Kijiji cha Guta, wilayani Bunda, Masatu Wanjara na mkewe, Sherida Musibha, wamepokea vifaa saidizi vya kuwasaidia kutembea, baada ya kukumbwa na changamoto ya maradhi ya miguu kwa zaidi ya miaka miwili.
Msaada huo wenye thamani ya shilingi 250,000 umetolewa na taasisi ya The Desk & Chair Foundation na kukabidhiwa Aprili Mosi,2025 kwa wanandoa hao, ambavyo vitawasaidia kutembea kwa urahisi tofauti na awali.
Masatu ameeleza furaha yake kwa kupokea msaada huo na kumshukuru mfadhili kwa kuguswa kutoa vifaa hivyo,baada ya kutumia mikongojo kwa muda mrefu kutokana na maradhi hayo.
Amesema ni kipindi muafaka kwa msaada huo kuwafikia kwani yeye na mkewe walikuwa wamesumbuliwa na maradhi ya miguu kwa zaidi ya miaka miwili,ambapo alikumbwa na jeraha lililosababishwa na maradhi kwenye mguu wake wa kushoto, huku mkewe akitumia kiti cha miguu minne kumsaidia kutembea.
Hata hivyo, Masatu ameeleza kuwa licha ya kupokea msaada huo, bado anasumbuliwa na maradhi ya tumbo ambayo yanapozidi, humfanya kupoteza fahamu,hivyo ameiomba Serikali kumsaidia kupata matibabu ya kibingwa kwani yeye na mkewe ni wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 80.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Alhaji Dk. Sibtain Meghjee, amesema kuwa alipokea picha kupitia WhatsApp ikimuonesha Masatu na mkewe wakikabiliwa na changamoto ya kutembea.
Ameeleza kuwa taasisi yao inatoa msaada bila kubagua, kwa kuzingatia kauli mbiu yao ya “Iwe dhiki iwe faraja, tupo pamoja,” baada ya kuona picha hiyo, aliguswa na kutoa msaada wa vifaa saidizi vyenye thamani ya shi.250,000.
Dk. Meghjee amefafanua kuwa taasisi hiyo inajivunia kutoa misaada katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, maji, mikopo na ufugaji wa mbuzi, ili kusaidia watu wenye mahitaji na kupambana na umaskini.
More Stories
Serikali yatoa fursa kwa wahitimu kidato Cha nne 2024 kubadilisha Tahasusi
Masache asema CCM Mbeya kimepoteza mtu muhimu
Serikali kuhakikisha wananchi wanaboresha taarifa zao