March 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

The Desk and Chair yarejesha tumaini la kielimu kwa William

*Imemlipia ada ya chuo kwa mwaka mzima,yaahidi kuendelea kumlipia kwa miaka iliobaki

*William aishukuru Desk and Chair

*Amshukuru Mwandishi wa Timesmajira na waandishi wengine

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza

Tassisi isiyo ya kiserikali ya The Desk and Chair Foundation, imeamua kumlipia ada ya mwaka wa kwanza chuoni kijana William Kabashi, ambaye ndoto zake za kuendelea na elimu ya chuo zilikuwa zimeyeyuka kutokana na mazingira magumu ya maisha.

William ambaye mwaka 2024, alichaguliwa kujiunga na Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Tabora, lakini hali ngumu ya maisha ilimfanya ashindwe kuendelea na masomo kwa wakati,hali hiyo ilimlazimu kutafuta msaada kupitia waandishi wa habari mwanzoni mwa mwaka 2025,ambao walioguswa na kisa chake na kuamua kumsaidia.

Akizungumza na waandishi wa habari William,amesema hatua hiyo ni kama ndoto iliyotimia, kwani alipoteza matumaini ya kuendelea na elimu ya chuo baada ya mama yake mzazi kufariki dunia akiwa bado yupo kidato cha kwanza.

“Baada ya mama kufariki, maisha yangu yalibadilika kabisa nilibaki peke yangu nikihangaika kutafuta namna ya kuendelea na shule kwa muda wote wa sekondari.Nilijitafutia vibarua ili niweze kumaliza masomo yangu. nimehitimu kidato cha nne mwaka 2023 na kupata daraja la tatu(division three),”amesema William na kuongeza:

“Namshukuru Mungu kwa kuwa waandishi akiwemo wa gazeti la Majira na Timesmajira Mkoa wa Mwanza,walikuwa kama mwanga mpya katika maisha yangu walinitafutia misaada na hatimaye wakaniunganisha na The Desk and Chair Foundation.Nilijiunga rasmi na chuo Machi mwaka huu na sasa ninaendelea na masomo kwa bidii, nawaomba Watanzania waendelee kuniunga mkono kwa miaka miwili iliyosalia ili niweze kutimiza ndoto zangu,”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa The Desk and Chair Foundation, Sibtain Meghjee, amesema taasisi hiyo imeguswa na juhudi za kijana huyo pamoja na changamoto alizopitia, hivyo wakaamua kumsaidia kwa moyo wa huruma na upendo.

“Tulipopata taarifa za kijana huyu kupitia kwa waandishi wa habari, tuliguswa,hivyo tulishirikiana na wadau wengine na leo tumekamilisha malipo ya ada ya mwaka wa kwanza iliyokuwa imebaki kiasi cha shilingi 370,000.Tunampongeza kijana huyu kwa juhudi zake na nia ya dhati ya kuendelea na masomo,”amesema Meghjee na kuongeza:

“Waandishi wamefanya kazi kubwa,bila wao, huenda taarifa hii isingetufikia,tunaamini kwa kushirikiana kama jamii, tunaweza kuokoa maisha ya vijana wengi wenye ndoto kubwa lakini waliokata tamaa kwa sababu ya kukosa msaada,”.

Meghjee amesisitiza kuwa taasisi yake itaendelea kumfuatilia kijana huyo na kutoa ushirikiano katika mwaka wake wa pili na wa mwisho wa masomo huku akiwahimiza wale wanaomsimamia kuhakikisha anamaliza vizuri.

“Tunajivunia kumuona kijana huyu akisonga mbele ameonesha ari ya kujifunza na tunataka awe mfano kwa wengine. Tunaomba taarifa za vijana wengine wenye mahitaji kama haya zifikishwe kwetu, bila kujali dini, rangi au kabila, ili nasi tuweze kuwasaidia,”amesema Meghjee.

Kwa hatua hiyo, kijana huyo sasa anaendelea na masomo yake kwa matumaini mapya, akiamini kuwa safari yake ya elimu itafika mbali kwa msaada wa watu wenye moyo wa huruma na upendo kama walivyoonesha The Desk and Chair Foundation pamoja na waandishi wa habari.