Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Tabora
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB),imeendesha mafunzo ya siku moja kwa wanahabari wa Mkoa wa Tabora na kuwataka kutoandika habari zenye mlengo wa kuchochea vurugu, ubaguzi au chuki miongoni mwa jamii.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) anayeshughulikia Elimu kwa Umma na Mawasiliano,Zawadi Msalla,amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea uelewa waandishi wa habari,kuhusu haki na wajibu wao kwenye kampeni zinazoendelea sasa na wakati wa uchaguzi mkuu,ili waweze kuripoti kikamilifu maudhui ya kampeni na uchaguzi mkuu’, ameeleza.

Ambapo amesisitiza kuwa katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea kwenye uchaguzi mkuu waandishi wa habari wana wajibu wa kuripoti habari na matukio yote ya kampeni kwa usahihi pasipo shaka yoyote.
Msalla amewataka kujikita zaidi katika kuimarisha amani, utulivu na demokrasia kupitia kalamu zao na kuchukua tahadhari dhidi ya matumizi mabaya ya majukwaa ya habari ikiwemo mitandao ya kijamii.
“Ninajua mnaelewa vizuri nini mnachopaswa kufanya katika kipindi hiki, epukeni kuchapisha au kutangaza habari zenye nia ya kuchochea vurugu, ubaguzi au chuki za kisiasa, kikabila, kidini au kijamii,”amesisitiza Msalla.
Amesisitiza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kutimiza wajibu waliowekewa kisheria, kwa kutoa taarifa zilizo sahihi na zisizo na upendeleo wowote ili kuimarisha amani na ulinzi wa haki za binadamu katika kufanya maamuzi.
“Vyombo vya habari ni daraja muhimu sana kati ya wagombea, vyama vya siasa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na wananchi hivyo vina nafasi ya kipekee ya kuwezesha upatikanaji taarifa sahihi za wagombea wote kwa jamii,”amesema.

Akitoa mada katika mafunzo hayo Ofisa Uchunguzi Mkuu wa THBUB,Innocent Aman ameeleza kuwa ibara ya 25-28 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi wajibu wa wanahabari kuripoti kampeni kwa usawa.
Amesisitiza kuwa kupitia uchaguzi, wananchi hutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka, hivyo ni jukumu la wanahabari kuripoti kwa usahihi maudhui ya mikutano ya kampeni hadi uchaguzi mkuu.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina