November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TGNP yampongeza Samia kufanyia kazi kilio cha kikokotoo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP,) umempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kufanyia kazi kilio cha kikokotoo kwa wastaafu na kufanya marekebisho kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40, jambo ambalo litaleta ahueni kwa wastaafu.

Hayo yamesemwa naMkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam katika kijiwe cha kahawa kilichoandaliwa TGNP Mtandao kwa ajili ya kufuatilia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Bajiti hiyo iliwasilishwa na Waziri wa Fedha Juni 13 na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Alisema marekebisho kwenye kikokotoo ni kitu kizuri, kwani wastaafu watakwenda kupata fedha zao walizofanyia kazi kwa muda mrefu.

“Watu wengi walitegemea kupanda kwa kikokotoo mpaka asilimia 50, kwani hizi ni fedha za watu walizozifanyia kazi kwa muda mrefu muhimu wapate fedha zao,”alisema Liundi

Hivyo aliiomba Serikali iendelee kufikiria zaidi kuendelea kupandisha kikokotoo kwa kiwango kikubwa.

Katika hatua nyingine Liundi alisema bajeti kuu ya Serikali haijawa na jicho la kijinsia, kwani wao walitarajia iwe na mrengo wa kijinsia zaidi hasa katika kukamilisha Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025.

“Licha ya Serikali kuyafanyia kazi baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakionekana.kuna changamoto hazijafanyiwa kazi kwenye bajeti kuu ya Serikali, kwani haijawa na jicho la jinsia kwa kiwango tulichokuwa tukitarajia,”alisema Liundi

Naye mdau wa masuala ya kijinsia, Mophat Mapunda, ameipongeza Serikali kurudishwa kodi za ardhi na majengo katika mamlaka za halmashauri ambapo itasaidia kujitanua kimapato katika vyanzo vya ndani na kuanzisha maendeleo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi TGNP, Gemma Kilimali ambaye ni mwanaharakati wa siku nyingi wa kutetea haki za wanawake nchini,ameomba Bajeti hiyo iende kutatua changamoto zinazomkabili Mtanzania na isiwe ya kisiasa.

Alisema bado Mtanzania anakumbana na changamoto zinazomkabili na kutaka bajeti ikaenda kutatua matatizo.