January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TFRA yabainisha fursa za uwekezaji tasnia ya mbolea

Yaratibu ushirikiano baina ya wafanyabiashara wa mbolea Tanzania na Urusi

Na Mwandishi wetu Timesmajira Online online

IMEELEZWA kuwa, Tanzania imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa sekta zote za kiuchumi,uzalishaji na tasnia ya mbolea ikiwemo.

Hayo yameelezwa Februari 15, 2024 na Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Mashariki Daniel Maarifa wakati akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent,katika kikao cha mtandaoni (video round table) baina ya wafanyabiashara wa mbolea wa Tanzania na wa nchini Urusi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kituo cha Utamaduni cha Urusi kilichopo Upanga, jijini Dar es Salaam.

Daniel Maarifa(kushoto), Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Mashariki akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, wakati wa kikao cha mtandaoni (video round table) baina ya wafanyabiashara wa mbolea wa Tanzania na wa nchini Urusi

Maarifa amesema, kikao hicho ni mwanzo wa uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili utakaopelekea kuingizwa kwa tekinolojia mpya kwenye sekta ya kilimo hususani tasnia ya mbolea hivyo tija kuongezeka kwenye sekta hiyo.

Aidha, Maarifa amewahakikishia wafanyabiashara wa Urusi upatikanaji wa malighafi za viwanda kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa madini ya fosifeti ujazo wa tani 375.1, gesi asilia tani za ujazo trilioni 57, uwepo wa makaa ya mawe ya kutosha, madini ya chokaa na madini mengine yaliyotawanyika maeneo tofauti nchini.

Akizungumza wakati wa mahojiano na waandishi wa habari, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan amesema, Tanzania imeonesha uwepo wa fursa za uwekezaji wa viwanda vya mbolea nchini.

Hivyo kikao hicho kimelenga kuweka daraja baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Urusi ili waweze kuja kuwekeza katika ujenzi wa viwanda pamoja na kushirikiana kwenye biashara ya mbolea.

Amesema, kwa mtazamo wake kwa namna nchi ya Tanzania na nchi jirani za Afrika Mashariki zilivyo, fursa zipo nyingi sana za kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea na kueleza ubalozi wake utaweka nguvu kubwa katika kuhakikisha uhusiano huo wa kibiashara baina ya Tanzania na Urusi yanafikiwa.

Elizabeth Muzo,Ofisa Uhamasishaji na Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) akizungumza jambo wakati wa kikao cha mtandaoni baina ya wafanyabiashara wa mbolea wa Tanzania na Urusi kilichofanyika katika Kituo cha Utamaduni cha Urusi kilichopo Upanga jijini Dar es Salaam

Kwa upande wake, Elizabeth Muzo, Ofisa Uhamasishaji na Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ametoa mwaliko kwa wawekezaji kuja kuwekeza nchini na kueleza uhakika wa kuwafikia watu milioni 400 kwa Tanzania na kwa soko la nchi zilizopo chini ya jangwa la Sahara takribani zaidi ya watu milioni 600.

Aidha, Muzo ameeleza kuwa, kupitia ofisi yake, Tanzania iko radhi kutoa ardhi kwa ajili ya kufanikisha uwekezaji wao ikiwa ni pamoja na kutoa misamaha ya ushuru wa forodha kwenye mitambo na mashine za viwandani.