January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TFRA kuwanufaisha wakulima na mbolea ya Ruzuku

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya

MKURUGENZI wa Mamlaka ya Udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA),Dkt. Stephan Ngailo amesema.serikali imeimarisha upatikanaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima kwa wakati ili waweze kufanya shughuli zao za kilimo mara msimu wa mwaka huu unapoanza.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya wakulima Nane nane yanayofanyika katikwa viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.

Amesema,katika kuhakikisha hilo linafanikiwa Taasisi hiyo imeweka mfumo thabiti wa wakulima kujiandikisha kuanzia katika ngazi ya vijiji ili waweze kupata mbolea hiyo.

Dkt.Ngailo ametumia nafasi hiyo kuwataka wakulima wajitokeze katika maeneo yao ili wajiandikishe hatua itakayowawezesha kupata mbolea hiyo wakati utakapofika.

Amesema, kuanzia Agosti 15 ma 16 wanatarajia kutangaza tenda ya ruzuku ya mbolea kwa wakulima.

 Mkurugenzi huyo amesema,hatua hiyo inalenga kuondoa kero,zilizojitokeza katika mifumo ya ruzuku iliyopita ikiwa ni pamoja na ucheleweshaji wa mbolea kwa wakulima.

“Serikali imeandaa mfumo wa kielektroniki ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kuziba mianya ya ubadhilifu hivyo wasambazaji.wasitarajie kupata chochote,”amesema Dk Ngailo.

Hata hivyo Dkt Ngailo alisisitiza kuwa katika kukabiliana na changamoto zilizojitokeza katika mifumo ya ruzuku iliyopita,serikali imejipanga vyema kuhakikisha mbolwa inawafikia wakulima kwa wakati sahihi.

Alisema lengo la kufanya  usajili wa waingizaji, wasambazaji, wauzaji wa mbolea pamoja na wakulima ni kutaka wote kunufaika na mbolea hizo za ruzuku.

“Mfumo huo utatumika katika kuhakikisha huduma

zote za usambazaji wa mbolea za ruzuku unatolewa na mtu sahihi na

kumfikia mkulima mwenyewe na siyo vinginevyo.

 “Serikali imejipanga kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi kwa ufasaha

ili mkulima aweze kunufaika na ruzuku ya mbolea ambayo inatolewa

“alisema Dkt. Ngailo.

Kuhusu namna usajili utakavyofanyika, Dkt  Ngailo amesema Usajili utafanywa na Afisa ugani waliopo katika ngazi za kata na vijiji na

kuthibitishwa na Mwenyekiti wa kijiji na baadaye taarifa za mkulima

kuingizwa katika mfumo wa kielectroniki ili kuwezesha usambazaji wa

mbolea hizo.

 Hata hivyo ameongeza kuwa,mzalishaji au mwingizaji wa mbolea nchini

atatumia mifuko maalum kwa ajili ya ruzuku yenye QR code  na maandishi

yanayosomeka ruzuku ili kuutambulisha kuwa mbolea hiyo inanunuliwa na

mkulima kwa bei ya ruzuku. 

Kwa mujibu wa Ngailo  utoaji wa ruzuku za mbolea ni matokeo ya maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kuona umuhimu wa kuwawezesha wakulima kulima kwa tija na kupelekea uhakika wa mavuno ya chakula na biashara kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Amesema, kiasi cha shilingi bilioni 150 za kitanzania

zimetengwa ili kutumika kutoa mbolea za ruzuku kwa wakulima kwa Mwaka

wa Fedha 2022/2023.