December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TFF kumpeleka Eymael FIFA

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema lipi mbioni kuwasilisha taarifa za kocha mkuu wa Yanga, Luc Eymael kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) juu ya matamshi ya kibaguzi aliyoyatoa kwa washabiki wa timu hiyo.

Taarifa iliyotolewa leo na Ofisa Habari wake, Cliford Ndimbo, imesema kuwa, limeamua kupeleka taarifa hizo katika vyombo husika ili nalo limchukulie hatua, kwa vile Kocha huyo bado anaweza kufanya vitendo hivyo katika nchi nyingine.

“Tutawasilisha taarifa hii FIFA juu ya kauli alizotoa Eymael ili nalo limchukulie hatua kwa vile kocha huyu bado anaweza kufanya vitendo hivyo katika nchi nyingine,”amesema Ndimbo.

Amesema, mwaka jana, FIFA ilifanyia marekebisho Kanuni zake za Nidhamu na kuongeza adhabu kwa wanaofanya vitendo vya kibaguzi kwa vile ni ukiukwaji mkubwa wa haki za msingi za binadamu.

Kwa mujibu wa Ibara ya 4 ya Katiba ya FIFA, vitendo vya kibaguzi vya aina yoyote ile haviruhusiwi katika mpira wa miguu.