Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa ameitaka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kuendelea kutekeleza kikamilifu jukumu lake la msingi la utoaji wa elimu ya watu wazima hadi katika ngazi ya Wilaya.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi Kongamano la Kimataifa la kuadhimisha miaka 50 ya elimu ya watu wazima ambapo amesema ni vizuri taasisi hiyo ikatumia maafisa elimu ya watu wazima waliopo kwenye Halmashauri kwa kuwapelekea programu za elimu ya watu wazima ili wakazitekeleze.
Kiongozi huyo pia amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini kuhakikisha wanafufua madarasa kwa ajili ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA) ili kusaidia kupunguza ongezeko la watu wazima wasiojua kusoma na kuandika.
“Naagiza madarasa ya MEMKWA yahuishwe. Wakuu wa Mikoa na Wilaya fuatilieni kuiona elimu ya watu wazima inahuishwa ili kupunguza au kuondoa kabisa changamoto ya kutokujua kusoma na kuandika na iwe sehemu ya ajenda mnapofanya ziara zenu,” amesema Waziri Mkuu.
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema, wizara anayoisimamia inatambua umuhimu wa elimu ya watu wazima katika kuleta maendeleo ya nchi hususan katika dhamira ya kuhakikisha kila mwananchi anajiletea maendeleo yake mwenyewe kwa kutumia rasilimali zilizopo ili kuleta maendeleo ya Taifa.
Amesema, watu wazima ndio washiriki zaidi katika shughuli za uzalishaji mali hivyo ili kuleta tija inayokusudiwa, vijana na watu wazima wote hawana budi kuwa na elimu na ujuzi wa kutosha.
Ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wanaoendesha elimu ya mafunzo ya watu wazima kutambua kuwa Serikali ilishafanya uamuzi kutumia shule za msingi na sekondari kama vituo vya elimu ya watu wazima, hivyo palipo na uhitaji wa elimu hiyo shule za msingi zitumike sambamba na vituo rasmi ambavyo vinakuwa vimeanzishwa kwa ajili hiyo.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini