Na Samwel Gasuku,TimesMajira,Online, Morogoro
TAASISI ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) inaendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakufunzi Wakazi wa mikoa kuhusu mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari kwa njia Mbadala (SEQUIP-AEP) unalenga kunufaisha wasichana 12, 000 hapa nchini ambapo kila mwaka utasajili wanafunzi 3,000 kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2022 hadi 2025 .
Mafunzo hayo ya siku tano yamefunguliwa rasmi leo mjini Morogoro na Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dkt. Naomi Katunzi.
Dkt. Katunzi amewataka Wakufunzi Wakazi wa mikoa kufuatilia mafunzo hayo ili yaweze kuwaongezea ujuzi na weledi katika kusimamia na kuendesha mradi huo kwenye mikoa yao ili waweze kutambua na kusajili wasichana wanaolengwa na mradi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Dkt. Michael Ng’umbi amesema mradi wa SEQUIP unaanza wakati maandalizi mengi tayari yamefanywa.
Pia, amesema kuwa miongozo ya wawezeshaji, mihtasari na moduli za masomo pamoja na vibali vya ujenzi ni baadhi ya maandalizi yaliyo tayari.
Aidha,Dkt. Ng’umbi amesema washiriki wa mafunzo haya ni wahusika wakubwa katika utekelezaji na amewaelekeza mara wamalizapo mafunzo waende moja kwa moja mikoani mwao kuanza utekelezaji.
Naye,Makamu Mwenyekiti ya Baraza la Usimamizi la TEWW, Profesa Sotco Komba amesema kutekeleza mradi wa kitaifa kunahitaji wahusika wakuu wote kuwa na uelewa mmoja na ndio maana mafunzo haya yameandaliwa. Pia, amehimiza washiriki kujadili na kuweka maazimio juu ya namna nzuri ya kuandaa walimu na kuwafundisha wanafunzi inavyopaswa.
Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (SEQUIP-AEP) unatekelezwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) chini ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TEMISEMI) na Benki Dunia.
Mradi huu umelenga kuwapatia elimu ya sekondari bila malipo wasichana waliokatisha masomo ya elimu ya sekondari kwa sababu mbali mbali kama vile kupata ujauzito au hali ngumu ya maisha wenye umri kati ya miaka 13 hadi 20.
More Stories
Walimu S/ Sekondari Ilala wafundwa juu ya maadili ya wanafunzi
Dkt. Samia afungua skuli ya sekondari Misufini, Bumbwini
Rais Mwinyi: Barabara Pemba zitajengwa kwa lami