October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TET yaendelea kutoa elimu kuhusu muundo wa mtaala wa Elimu

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imeendelea kutoa elimu kuhusu muundo wa mtaala wa elimu ulioboreshwa katika Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (DITF) maarufu kama Sabasaba, yanayoendelea katika viunga vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika Maonesho hayo leo, Mkuza Mitaala kutoka TET, Augusta Kayombo amesema watanzania watakaofika katika banda lao watapatiwa machapisho ya kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita.

Amesema machapisho hayo pia ni kwaajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu hasa wenye uoni hafifu, na kwamba katika muundo wa mtaala ulioboreshwa, utaanza na elimu ya malezi ambao utatolewa kwa miaka miwili kwa mtoto anaeanzia miaka mitatu.

“Mwanafunzi ataingia katika elimu ya awali ambayo itatolewa kwa mwaka mmoja, akitoka ataenda kusoma darasa la kwanza hadi sita, na akienda sekondari atachagua mkondo wa amali au jumla.“Akichagua wa amali atasoma kwa miaka minne kwa kutumia mtaala wa TET utakaojumuisha masomo ya historia ya Tanzania na maadili, kingereza, hisabati na elimu ya biashara,” amesema.

Akifafanua zaidi amesema mtoto atatakiwa kuchagua fani moja kutoka veta ambayo atabobea katika kuisoma na atatahiniwa na Baraza la Ufundi la Taifa (NACTVET) na kwa masomo aliyosoma kwa mtaala wa TET atatahiniwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).

Amesema mwanafunzi atakuwa na vyeti viwili vya uhitimu, kitakachotolewa na NACTVET na cha uhitimu wa mitihani atakachopatiwa na NECTA, na kwamba katika mkondo wa jumla atasoma kwa miaka minne na kutakuwa na michepuo 11.

Kayombo amesema katika michepuo mwanafunzi atachagua kulingana na umahiri anaotarajia kuujenga, pamoja na masomo ya lazima ambayo ni Geografia, elimu ya biashara, hisabati, kingereza, Kiswahili na historia ya Tanzania na maadili.“Muundo wa mtaala huu unamruhusu mtoto kusoma pande zote mbili kwa mfano aliehitimu kidato cha nne mkondo wa amali anaruhusuwa kwenda kuendelea na elimu ya jumla kwa kidato cha tano na sita, kulingana na fani alizozisoma,” amesema Kayombo.