December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tembo wavamia Igunga, waharibu hekari 66 za mazao

Na Jumbe Ismailly, TimesMajira Online, Igunga

KUNDI la tembo wanaokadiriwa kufika 800 wamevamia katika Kata ya Igoweko,wilayani Igunga,Mkoani Tabora na kisha kula hekari 66 za mazao ya chakula yakiwemo mahindi,mtama pamoja na mpunga na kusababisha kaya 50 za kata hiyo kukosa chakula.

Akitoa taarifa hizo kwenye mkutano wa baraza la madiwni wa Halmashauri ya wWlaya ya Igunga,Diwani wa Kata ya Igoweka,Omari Hamisi amefafanua kwamba kundi hilo la tembo liliingia katika vitongoji viwili vya Igoweko “B”na Bugingija “D” na kula mazao ya wananchi waliokuwa hawajavuna na hivyo kusababisha kaya 50 kukosa chakula.

Kwa mujibu wa Hamisi kufuatia hali hiyo ndipo alipoiomba Serikali kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kuwatoa tembo hao ili wasiweze kuendelea kuleta madhara kwa wananchi sambamba na kuwalipa fidia wananchi walioathirika.

Naye ofisa Maliasili wa Wilaya ya Igunga,Jahulula Edward amethibitisha kundi la tembo hao kuvamia makazi ya watu na kuharibu hekari 66 za mazao ya chakula na kwamba kati ya hekari hizo,hekari 42 ni za mahindi,hekri 17 ni za mtama na hekari 7 ni za mpunga lakini hakuweza kutaja thamani ya mazao yaliyoathiriwa na wanyama hao.

Hata hivyo Edward amesisitiza kwamba tayari ameshawasiliana na Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Magharibi ambacho kinatarajiwa kuwasili haraka katika eneo la Kata hiyo kwa ajili ya kuwaondoa tembo hao na kuwarudisha katika msitu wa Hifadhi wa Unyambiu.

Aidha Ofisa maliasili huyo amesema kwamba idadi ya tembo imezidi ukubwa wa eneo la Hifadhi hiyo kutokana na tembo wengi kutoka ndani ya Hifadhi na kuhatarisha usalama wa wananchi pamoja na mali zao.

Amefafanua Ofisa huyo wa maliasili kuwa msitu wa hifadhi wa Unyambiu wenye ukubwa usiopungua hekari 25 unakadiriwa kuwa na tembo wasiopungua 800 na hivyo kutumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kuwa makini na kuondokana na tabia ya kuwachokoza wanyama hao.