June 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Teknolojia yawezesha wastaafu kupata huduma za PSSSF kwa urahisi

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online – Mwanza

Kukua kwa teknolojia kumerahisisha  utendaji kazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), huku ukileta  unafuu kwa wastaafu wanaohitaji huduma katika mfuko huo.

Akizungumza jijini Mwanza,Juni 12,2025 wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kutoka Mkoa wa Mwanza, Kaimu Meneja wa PSSSF Kanda ya Ziwa Mashariki,Happiness Manyenye,amesema kupitia teknolojia, sasa huduma  zinapatikana kwa njia ya kidijitali kupitia mfumo wa ‘PSSSF Portal’ na ‘PSSSF Kiganjani’.

“Kwa sasa mwanachama anaweza kujisajili, kuona michango yake, na hata kuwasilisha maombi ya malipo kupitia simu ya mkononi bila kufika ofisini,” amesema Manyenye na kuongeza:

“Pia, mwanachama anaweza kubadilisha majina au kujihakiki baada ya kuthibitishwa mara ya kwanza kupitia mfumo huo wa kidijitali,”.

Aidha,Manyenye, ameeleza kuwa licha ya faida hizo, maendeleo ya teknolojia yameambatana na changamoto za kiusalama, ikiwemo vitendo vya utapeli kwa wastaafu  ambao baadhi wamekuwa wakitumiwa ujumbe mfupi wa simu.

“Tunatoa elimu kwa wanachama kuwa makini na utapeli,na wasitoe taarifa zao kwa namba binafsi ambayo imemtumia  ujumbe hata kama umetaja ‘check namba ‘ yake,kwani ujumbe  kutoka PSSSF hutumwa ukiwa na jina la taasisi, si namba binafsi. Wanachama wakipokea ujumbe wenye kwa namba binafsi , wanashauriwa kufika ofisini kuthibitisha,”.

Kwa mujibu wa Manyenye, tayari baadhi ya kesi za utapeli zimeripotiwa kwa upande wa PSSSF  Kanda ya Ziwa Mashariki, ambapo taarifa nyingi zimeripotiwa na wanachama waliopokea ujumbe unaodai unaotaja  ‘check no’ au taarifa nyingine.

Pia amesema,katika maboresho ya huduma, kuanzia Januari 2025, PSSSF imeongeza kiwango cha chini cha pensheni ya kila mwezi kutoka shilingi 100,000 hadi 150,000. Pia, imeanzisha fao la msaada wa mazishi, ambapo familia ya mstaafu aliyefariki itapatiwa msaada huo.

Vilevile, malipo ya pensheni kwa wastaafu yataendelea kulipwa kwa miezi 36 baada ya kifo cha mstaafu, na yatarithiwa na mwenzi wa ndoa au watoto walio chini ya umri wa miaka 21.

Kwa upande wake  Muuguzi Mstaafu  Jane Kalimasi kutoka mkoani  Mwanza, amesema huduma za kidijitali zimeondoa usumbufu wa kusubiri kwa muda mrefu kupata huduma.

“Kupitia simu, naweza kupata taarifa zote muhimu kuhusu pensheni yangu,kuhakiki taarifa zangu pia PSSSF wamekuwa wakitutumia ujumbe mara kwa mara wa kutukumbusha. Hii ni msaada  kwetu wastaafu,kwani tunakuwa na mambo  yanayotufanya kusahau,”.

Hata hivyo, amesema jambo analojivunia zaidi kwa PSSSF,ni kuaamini wastaafu na kuwakopesha.

Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko, amewahimiza waandishi wa habari kuandika zaidi kuhusu mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuwahamasisha wananchi kujiunga na kufaidika na huduma hizo.