December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Teknolojia mpya ya bajaji,pikipiki zinazotumia mfumo wa umeme kuanza kazi jijini Tanga

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online Tanga

Vijana 75 kutoka Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na SIDO jijjni Tanga wamepatiwa mafunzo ya namna ya utumiaji wa teknolojia mpya ya vyombo vya moto ikiwemo bajaji na pikipiki zinazotumia mfumo wa umeme jijini Tanga.

Kati ya vijana hao 40 wametokea VETA mkoani Tanga na wengine 35 kutoka SIDO huku baadhi kutoka gereji jijini humo.

Mafunzo hayo yametolewa June 25 mwaka huu juu ya namna ya matumizi ya bajaji hizo yaliyoandaliwa na shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Open Innovation chini ya kampuni ya ROBOTECH LABS.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, 0fisa mradi huo Abdulwahab Issa amesema vijana hao wamejifunza na kuona namna bajaji hizo zinavyofungwa pindi zinapotoka viwandani lakini pia wameweza kujionea mifumo ya umeme na mota vinavyofanya kazi pamoja na kutengeneza na kutumia vyombo hivyo.

“Bajaji hii ina uwezo wa kutembea kilomita 80 hadi 100, kwa chaji iliyojaa kwa asilimia 100 kwa umeme wa sh 3,000 hapo inaweza ikatuonesha kwamba ni namna gani unaweza kwenda ukaokoa kipato chako cha matumizi katika ununuaji wa mafuta,”amesema.

Sambamba na hayo, wamelenga kutoa mafunzo kwa vijana hao ili kupata mafundi watakaoweza kujua jinsi ya uendeshaji, uundaji pamoja na urekebishaji wa vyombo hivyo na wasambazaji kama bidhaa zitakapotoka viwandani.

“Wito wangu kwa vijana wa Mkoa wa Tanga, waendelee kujitokeza pale fursa hizi zitakapotokea, ni adimu na ni mara chache zinapokuwa zinatolewa bure kwa sababu hakuna gharama zozote wanazolipia, waje wajionee, wajifunze ili waweze kuwa mafundi, madereva na wasambazaji wa huduma za bidhaa hizi za bajaji,”.

Hata hivyo amebainisha kuwa zaidi ni jitihada za utunzaji wa mazingira kuhakikisha nchi inatoka kwenye matumizi ya nishati chafu na kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi hivyo kulenga kuanza kutumia tekinolojia ya nishati ya umeme na kuachana na matumizi ya mafuta.

Baadhi ya walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kwamba mafunzo hayo yamewapa mwangaza na kuona ni jinsi gani teknolojia hiyo inaenda kuwafanikishia katika kipato chao pindi watakapotumia bajaji hizo.

Kwa upande wake Ofisa Vijana kutoka Halmashauri ya jiji la Tanga Fadhili Secha amesema teknolojia hiyo inakwenda kuwarahisishia vijana matumizi makubwa ya nishati ya mafuta ya petroli na kuwasaidia kupata faida wanapoendesha shughuli zao za usafirishaji.

Mwenyekiti wa waendesha bajaji Mkoa wa Tanga Rahimu Makange amesema mafunzo hayo ni fursa kwao na bajaji hizo zimerahisisha mambo mengi.

Naye Halfani Rashidi dereva wa bajaji jijini Tanga amesema,ameishaanza kuitumia bajaji hiyo ya umeme na manufaa yake ni makubwa.

“Bajaji ya kawaida nilikuwa natumia zaidi ya sh 15,000 kwa siku lakini hii natumia umeme wa sh 3,000 kwa siku ni rahisi,hazina gharama kubwa, ni suala la kuhakikisha tu hukosi luku, lakini suala la kuingia sheli kupanga foleni kutafuta petroli au dizeli hakuna,” ameeleza na kuongeza kuwa

“Unapokuwa na umeme wa sh 3,000 unaweza ukasafiri kutoka Tanga hadi Korogwe, lakini ni petroli matumizi yangekuwa makubwa,”.


Teknolojia mpya ya matumizi ya bajaji za mfumo wa umeme inatajwa kwenda kuongezea kipato vijana wengi lakini pia inakwenda kuwaondolea gharama za nishati ya mafuta watumiaji wa vyombo hivyo.