November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TEF yawasilisha serikalini mapendekezo ya marekebisho ya sheria za habari

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limekabidhi serikalini mapendekezo ya
marekebisho ya sheria mbalimbali zinazogusa sekta ya habari nchini.


Mapendekezo hayo yanagusa sheria na/au baadhi ya vifungu vya sheria ambavyo
kwa mtazamo wa wadau wa habari nchini, vinakwaza kwa namna moja au nyingine
uandishi wa habari na vyombo vya habari katika utekelezaji wa majukumu yake.


Mapendekezo hayo yamepokewa leo (Jumanne Novemba 16, 2021) mjini Dodoma na
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Ashatu Kijaji kutoka
kwa Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile.


Akizungumza katika hafla hiyo, Balile amesema Muhtasari uliowasilishwa unalenga
kuiwezesha serikali kuzingatia mapendekezo ya wadau wa habari katika mchakato
wa marekebisho ya sheria husika, kabla ya kupelekwa bungeni kwa ajili ya kupata
baraka za Bunge.


“Sheria zilizochambuliwa katika muunganisho huu ni Sheria ya Huduma za Habari,
2016, Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa, 2016 na ile ya Mawasiliano ya Kielektroniki
na Posta; (Maudhui ya Mtandaoni) Kanuni, 2020 na Sheria ya Uhalifu wa Mtandao,
2015,”alisema Balile.


Alitaja baadhi ya mambo ambayo wadau wanaomba kufanyiwa marekebisho au
kubadilishwa katika Sheria hizo kuwa ni pamoja na mamlaka ya Ofisi ya Mkurugenzi
wa Idara ya Habari (Maelezo) ambayo inaweza kufungia vyombo vya habari
vinapodhaniwa au kutuhumiwa kuwa vimekosea, bila suala au makosa husika
kufikishwa katika vyombo vya kisheria vya kiuamuzi kama Mahakama.


“Wadau tunaona kuwa kifungu kama hiki kinamnyima mtuhumiwa nafasi ya
kujitetea na kinakiuka kanuni ya msingi ya chombo kusikilizwa kabla kuhukumiwa,”
alisema Balile.


Mwenyekiti huyo wa Jukwaa la Wahariri ametaja suala jingine kuwa ni Sheria ya
Huduma za Habari (MSA) kuanzisha vyombo vinne vya kusimamia sekta ya habari,
tofauti na sekta au taaluma nyingine ambako masuala husika husimamiwa na chombo
au mamlaka moja.


“MSA inaanzisha Accreditation Board (Bodi ya Ithibati), Mfuko wa kusomesha
waandishi wa habari na Independent Media Council (Baraza Huru la Habari), sisi
katika hili tunapendekeza kuwapo kwa chombo kimoja pekee cha kuratibu sekta
badala ya kuwa na vyombo vingi,” alisema.


Amesema mchakato mzima wa kupata maoni na mapendekezo yaliyowasilishwa,
umezingatia ushirikishwaji wa wadau wengine wa habari kupitia Umoja wa Haki ya
kupata taarifa (CORI) (ambao TEF ni mwanachama wake), ukiunganisha taasisi 11
chini ya Uenyekiti wa Baraza la Habari Tanzania (MCT).


Pamoja na TEF, wengine ni Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi
la Tanzania (MISA – TAN), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania
(TAMWA), Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Kituo cha Taarifa kwa
Wananchi (CIB), Twaweza, SIKIKA na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC).


Alisema katika mchakato huo pia kulikuwa na fursa ya kupata maoni ya Wahariri na
baadhi ya wawakilishi wa Vilabu vya Waandishi wa Habari vya mikoa (Regional
Press Clubs), katika kusanyiko lililoitishwa na TLS mjini Dodoma.


“Tulipata pia fursa ya kupata mawazo ya watu wenye uzoefu wa masuala ya habari
na taarifa kama Jenerali Ulimwengu na Mkurugenzi wa Jamii Media, Maxence
Mello,”alisema Balile.


Akizungumza baada ya kupokea Muhtasari wa mapendekezo hayo, Waziri wa
Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Kijaji amesema Serikali itayafanyia
kazi mapendekezo hayo kwa lengo la kuiwezesha sekta ya habari kuwa rafiki kwa
wadau wake, hususan waandishi wa habari.


“Lengo la serikali ni kuhakikisha kwamba sekta ya habari inakuwa rafiki na ni
dhamira yetu sote kupiga hatua na kufikia malengo ya ufanisi utakaokuwa na faida
kwa kila mmoja. Hatua ya leo ni mwanzo mzuri na ninaamini tutapiga hatua kwa
faida ya taifa letu,”amesema Dk. Kijaji.


Baada ya kupokea mapendekezo hayo, waziri huyo ameyakabidhi kwa Katibu Mkuu
wake, Dk. Zainab Chaula pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Jim Yonazi kwa ajili ya
kuanza kuyafanyiwa kazi.


“Kazi ndiyo imeanza, hakuna kusubiri, kwahiyo baada ya kuyapokea naomba na
mimi nikukabidhi Katibu Mkuu kwa ajili ya kuyafanyia kazi,”amesema Dk. Kijaji.