January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TEF yatoa pole, ajali ya ndege Precision Air

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limepokea kwa masikitiko vifo vya watu 19 waliokufa katika ajali ya ndege ya shirika la Ndege la Precision siku ya Jumapili Novemba 6, 2022.

TEF inatoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, pia tunawaombea wote walioumia wapone haraka. Kadhalika, tunatoa pole kwa Kampuni ya Precision na Watanzania kwa ujumla kutokana na janga hili.

Wakati huo huo, tukirejea matukio ya ajali yakiwamo hii ya ndege ya Precision, meli ya MV Bukoba, MV Spice Islander na nyingine zilizotokea majini, kimsingi zimepoteza maisha ya watu wengi kwa sababu ya uzembe na ukosefu wa vifaa vya uokoaji.TEF inatambua na kupongeza kazi kubwa ya uokoaji iliyofanywa na wavuvi wadogo katika ajali ya Precision.

Hii si mara ya kwanza kwa wavuvi kufanya kazi ya kishujaa ya uokoaji kama hii. Walifanya hivyo wakati wa MV Bukoba, MV Spice Islander na katika ajali nyingine ndogo ndogo za majini.

Kutokana na kazi ya uokoaji inayofanywa na wavuvi, TEF tunapendekeza wavuvi wote sasa waandaliwe kama Jeshi la Akiba la Uokozi kama ilivyo kwa Mgambo kwenye Jeshi la Nchi Kavu.

Wakati tukiendelea na maombolezo, tunaisihi Serikali ifanye uwekezaji mkubwa katika mafunzo na vifaa vya uokoaji zikiwamo helikopta kwani hakuna mwenye uhakika kuwa ajali ya Precision majini ndiyo itakuwa ya mwisho.

Mungu ibariki Tanzania.

Deodatus Balile,Mwenyekiti TEF