January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TEF waomboleza kifo cha Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Rais (mstaafu) wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi aliyefariki dunia Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam alikokuwa anapatiwa matibabu.

Salamu hizo za rambirambi zimetolewa leo na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile ambapo amesema Mzee Mwinyi katika uongozi wake alianzisha demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa Tanzania, aliondoa vikwazo kwa kampuni binafsi, akapunguza vikwazo vya uagizaji bidhaa kutoka nje, na kupata jina la utani la “Mzee Ruksa”, msemo wa Kiswahili ambao unaweza kutafsiriwa kama “Ruhusa ya Mheshimiwa kitenda lililo jema” na kuwafanya Watanzania wajue na kushika fedha katika uongozi wake.

Balile ameongeza kuwa, Mzee Mwinyi alisisitiza uwajibikaji kazini na kukemea wazembe, kwa kuasisi maneno “fagio la chuma” maana wazembe wote walikuwa wakiondolewa kazini au kupunguzwa kazi. Ndiye aliyeruhus watumishi kujitafutia kipato cha ziada baada ya saa za kazi madaktari wakaanza kufanya kazi kwenye vituo vingine na hata kufungua hospitali zao binafsi pia Aliamini katika ukuaji wa Uchumi kwa mtu mmoja mmoja kwa maendeleo ya familia na taifa.

Kadhalika, Balile amesema Mzee Mwinyi wakati wa uhai wake alichagiza michezo na yeye alikuwa mpenda michezo hasa jogging (kukimbia). Pia alikuwa mwandishi wa mashairi na vitabu.

Balile amesema kwa pamoja TEF wanaungana na familia ya Mzee Ali Hassan Mwinyi na Watanzania wote kuomboleza msiba huo mkubwa kwa taifa.

Mungu ailaze mahala pema peponi roho ya Mzee Mwinyi.