March 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Team nane kuchuana ” Bwigane Tv Ramadhan Street Cup”

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

KUPITIA Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, Bwigane Tv, imekuja na michuano ya mpira wa miguu itakayotambulika kama ‘Bwigane TV Ramadhan Street Cup’ itakayo anza rasmi kesho Machi 6, ikizishirikisha ‘Team’ nane zilizopo katika kata za Wilaya ya Ubungo.

Michuano hiyo itafunguliwa na Mgeni Rasmi, Katibu wa Chama cha Soka(Ubungo Football Associatian UFA) Wilaya ya Ubungo, Ruben Kaduguda, huku ‘Team’ hizo nane zikichezwa katika viwanja viwili tofauti, Makuburi External na uwanja wa Sahara uliopo Mabibo.

Akizungumza na Vyombo vya Habari, Mratibu wa michuano hiyo, Agnes Alcardo, amesema, lengo la michuano hiyo ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika upande wa michezo, ikiwa pamoja na kurudisha kwa jamii kupitia kipindi hiki cha mfungo.

Agnes amesema, michuano hiyo ya Mpira wa miguu itashirikisha ‘Team’ hizo nane ambazo ni Mabibo Boys, Nanga FC, Muonekano FC,Makuburi FC, Kibangu Rangers, Lacassa FC, TMC FC na EFCA FC( External Football Center Academy), timu ambazo zitagawanywa katika makundi A na B, huku timu ya ufunguzi ikiwa ni Mabibo Boys na Nanga FC.

Aidha amesema kuwa, katika kinyang’anyiro hicho, kwa mashindi wa kwanza atajinyakulia zawadi ya Mbuzi na Jezi na mshindi wa pili akiondoka na zawadi ya mipira na Jezi, ambapo pia kutakuwa na zawadi zitakazotolewa kwa Kipa Bora, Mfungaji Bora na Mchezaji Bora.

“Kama mnavyofahamu kuwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo amekuwa akileta hamasa hususani katika upande wa michezo kwa yale magoli ya Mama, hivyo na Bwigane Tv imeona ni vyema ikamuunga mkono Rais wetu katika kukuza na kuviendeleza vipaji vya vijana katika upande wa michezo.

Hivyo imekuja na michuano hii ya Mpira wa miguu, tukumbuke kuwa watu wapo katika mwezi wa mfungo hivyo ni lazima pia mazoezi yafanyike kwa ajili ya kuimarisha afya, hivyo niwakaribishe watu wote kuweza kushuhudia michuano hii ambayo itakuwa siyo ya kitoto! Zawadi zitakuwepo kwa washindi lakini pia kutakuwa na surprise mbalimbali watazipata watakaofika uwanjani”, amesema Agnes.

Pia ameeleza kuwa, kwasasa michuano hiyo imeanza katika Wilaya ya Ubungo, lakini hapo baadae lengo ni kuzifikia Wilaya zote Jijini Dar es Salaam, ili kukuza na kuibua vipaji katika mpira wa miguu, hivyo ametoa wito kwa wananchi wote hususani katika Wilaya ya Ubungo kujitokeza kwa wingi hapo kesho kuweza kushuhudia michuano hiyo pamoja na burudani  mbalimbali zitakazokuwa zikiendelea katika viwanja hivyo.

Mashindano ya Bwigane Tv Ramadhan Street Cup yanatarajiwa kuanza Machi 6 na kumalizika Machi 30, 2025 ambapo ndiyo itakuwa fainali.