Na Raphael Okello, Timesmajira Online,Musoma
MENEJA wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali amewataka watoa huduma kupitia mitandao kufuata sheria na kanuni za nchi ili kuepuka kuingia matatani na kukuza vyombo vyao kiuchumi.
Amewakumbusha waliosajiliwa na kupewa lesseni na TCRA kutoa huduma kupitia mitandao kuzingatia masharti ya leseni zao na sheria zinazosimamia huduma wanazozitoa kwa jamii.
Banali amezungumza hayo wakati akiwasilisha mada inayohusu shughuli za TCRA katika mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari mkoani Mara iliyofanyika mjini Musoma Aprili 13,2024 ambapo amesema TCRA haitawafumbia macho wanaoendelea kukiuka sheria na kanuni za huduma za mitandao,
Aidha amewashauri waandishi wa habari za kielektroniki kutumia vyombo vyao vya habari kupakia maudhui ambayo yataweza kuwainua kiuchumi badala ya kupakia maudhui yanayoleta ukakasi jambo alilosema haliwezi kuwasaidia.
Amesisitiza kuwa dunia imebadilika na kuingia katika mfumo wa kielektroniki hivyo ni vyema waandishi wa habari na jamii kwa ujumla kutumia mitandao kuzalisha bidhaa bora zinazovutia watumiaji.
“Kutokana na sensa ya mwaka 2022 idadi ya watanzania ni milioni 61 ukilinganisha na laini za simu milioni 73.1 zilizosajiliwa kufikia Desemba 2023 inaonesha dhairi kuwa jamii inahamia kwenye mawasiliano ya mitandaoni,” ameeleza na kuongeza kuwa
“Isitoshe, watumiaji wa Intaneti kufikia Desemba 2023 wamefika milioni 35.8 na akaunti za pesa mtandaoni zimefika milioni 52.9 , hii ni fursa,”.
Kwa sababu hizo amewataka waandishi wa habari kuhakikisha kuwa maudhui wanayopakia kwenye vyombo vyao vya mitandaoni zinawaingizia pia mapato kupitia data.
Amewataka waandishi wa habari kuhakikisha kuwa vyombo wanavyovitumikia vimesajiliwa na maudhui inayorushwa haikinzani na masharti na sheria za huduma husika.
Naye Ofisa Mawasiliano TCRA, Robin Ulikaye amevitaka vyombo vya habari kuacha kutoa matangazo bila kuzingatia sheria za uchaguzi.
“Kwa sasa tunaelekea kwenye chaguzi, vyombo vya habari mnapaswa kuanza kuwa makini katika mchakato wote hadi kufikia kutoa matokeo, epukeni kupakia maudhui yenye kuumiza au uchochezi wa kuleta uhasama na vurugu,”amesema Ulikaye.
Pia amewata waandishi wa habari kuwatendea haki wagombea kwa kuacha kurusha au kupakia taarifa binafsi za wagombea bali wajikite katika ilani za vyama na sera zao zenye kuwaletea maendeleo wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko, amewakumbusha waandishi hao kuzingatia sheria za huduma za vyombo vya habari, sheria za maudhui mtandaoni na posta(EPoca) na kuwataka wazingatie weledi wa taaluma za uandishi wa habari.
Amesema wakizingatia hayo hawataweza kuingia matatani wakati wote wanapokusanya na kutoa taarifa kwa jamii.
Nao waandishi wa habari waliopata mafunzo hayo wameipongeza TCRA kwa kuwafikia elimu hiyo muhimu na kwamba watazingatia wakati wote wanapokuwa kazini.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato