November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCCS kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika ufugaji

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

CHAMA cha Wafanyabiashra wa Ng’ombe Tanzania (TCCS) kimesema kinaendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan, za kuhakikisha sekta ufugaji nchini inazidi kuboreshwa na  kuwa ufugaji wa kisasa.

Akizungumza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maonesho ya mifugo na mnada yanayotarajia kufanyika Juni 14 -15,2024 maeneo ya Ubena Estate Chalinze, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Kibiashara wa Ng’ombe (TCCS) Naweed Mulla, amesema lengo programu hizo ni kusaidia wakulima na wafugaji kujikwamua kiuchumi wao wenyewe na kuongeza pato la taifa kupitia ufugaji.

Mulla amesema wanatoa wito kwa vijana wengi na wafugaji wapya wanaotamani kuingia katika tasnia hiyo ya ufugaji kushiriki  maonesho hayo ili kuweza kujifunza mambo mbalimbali juu ya ufugaji na kuona namna gani wataweza kufanya biashara hizo za kilimo.

Amesema takribani washiriki 300 wanatarajia kuhudhuria maonesho hayo ambayo yatafanyika ndani ya siku tatu katika viwanja hivyo, yakiwa na lengo la kuwawezesha wafugaji, wasindikaji na wadau mbalimbali nchini kushawishi sera za maendeleo na kukuza uzalishaji wa mifugo endelevu kwa njia ya kuwajengea uwezo na mitandao.

Amesema maonesho hayo yana nia ya kuwezesha jukwaa madhubuti la Kitaifa la wafugaji wasindikaji na wadau katika mnyororo wa thamani ya mifugo kutambulika kwa lengo moja la kuendeleza sekta hiyo kwa mbinu bora endelevu za kiuchumi na kimazingira.

“Tamasha hilo lilianzishwa na kuchukua nafasi yake kwa mara ya kwanza mwaka 2022 ambapo kwa mwaka huu linatarajia kufanyiwa maboresho makubwa ambayo yataenda sambamba na utoaji wa elimu ili kutoa msaada kwa jamii namna ya kufuga kwa tija,”amesema.

“Tunamshukuru Rais Samia  kwa kuweka mazingira bora ,rafiki na wezeshi kuhakikisha sekta hiyo inawakwamua wakulima na wafugaji kimaisha na kuhakikisha wanaongeza tija na ubunifu katika shughuli za kilimo,”amesema.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugezi Idara ya Mipango,Ushauri na Mahusiano ya Taasisi wa Benki ya Kilimo, Mkani Waziri, amesema wao kama benki kazi yao kubwa ni kutoa maendeleo katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi hivyo wameamua kushirikiana na TCCS kuona namna wanavyoweza kuleta mageuzi katika tasnia ya ufugaji.

Amesema wamekuwa washiriki wakuu katika tasnia ya ufugaji ili kuhakikisha Watanzania wanafuga kwa tija na kuweza kupata kipato cha  kugeuza maisha yao .

“Tunatoa  mikopo ya moja kwa moja kwa wafugaji ili kuwawezesha wafugaji ambapo hadi sasa benki imetoa sh. Bilioni 38 ya mikopo kwa wafugaji kwa wanufaika wapatao 8,688 katika mikoa 21,”alisema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoani Pwani, Ngobere Msamau, amesema kupitia maonesho hayo wanatarajia kupata  elimu ya kufanya wazidi kuongeza tija katika ufugaji wa kisasa na kuondokana na ule wa kienyeji.

“Kupitia Maonesho haya tunajifunza mambo mbalimbali ya ufugaji wa tija na wa asili na kuona namna gani wenzetu walivyopiga hatua katika ufugaji bora,”amesema.