November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCB  yajiimarisha ushindani,kutangaza bidhaa zake mpya za kidigitali 

Na Mwandishi wetu , Timesmajira 

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) ,imesema kuwa kwa sasa  imeimarisha nafasi yake katika ushindani wa soko,kwa kutangaza bidhaa zake mpya za kidigitali. 

Imesema bidhaa hizo mpya za Adabima na Kikoba zimebuniwa ili kukidhi mahitaji ya wateja yanayoendelea kubadilika siku hadi siku.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa,Mkuu wa Kitengo cha Bima Benki, Francis Kaaya amesema bidhaa ya ADABIMA ni mpango wa utoaji dhamana wa ada ambao TCB imeshirikiana na kampuni ya Metro Life Assurance ili kuwapa wazazi na walezi utulivu wa kiakili.

Amesema  mpango huo unahakikisha watoto wanaweza kuendelea na elimu yao hata pale wazazi au walezi wao wanapofariki au kupata ulemavu wa kudumu, na hivyo kulinda malengo yao ya kitaaluma.

,“Tunatambua umuhimu mkubwa wa elimu katika kujenga kesho bora ya jamii yetu hivyo bidhaa hii inawapa usalama wa kifedha pia inalea ndoto na matarajio ya wateja wetu,”amesema na kuongeza

“Bidhaa hii ni uthibitisho tosha wa dhamira ya TCB Benki ya kuwasikiliza na kuwahudumia wateja kadiri ya mahitaji yao na kuwahudumia Watanzania wote kwa ujumla,”amesema.

Aidha amesema bidhaa ya  KIKOBA ni mpya, rahisi na yenye ufanisi ya kuweka akiba mtandaoni ambayo inayoboresha dhana ileile inayotumika katika vikundi vilivyozoeleka vya kuweka akiba na kukopeshana. 

Amesema bidhaa hiyo ya kidigitali na ya kifedha, ikiwezeshwa na ushirikiano wa kimkakati ambao TCB ilifanya na kampuni za simu nchini, inawawezesha wateja kusimamia fedha zao kwa urahisi kutoka viganjani mwao.

Kwa upande wake  Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji wa Bidhaa za Kidigitali (Digital Product Operations Officer) ,Pray Henry Matiri, amesema  bidhaa ya Kikoba ni zaidi ya fursa ya kidigitali,kwani Kikoba inabeba dhana pana ya uwazi, ujumuishi, na usalama katika uwekaji wa akiba na usimamizi bora wa kifedha.

Amesema wakitumia nyenzo hiyo ya teknolojia, wanaviwezesha vikundi nchini kote kusimamia mategemeo yao ya kiuchumi, kukua kiuchumi na kujitegemea.

“Katika hotuba yake,  Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza umuhimu wa maonesho ya SABASABA katika kuleta maendeleo ya kiuchumi kwani amesema maonesho ya SABASABA ni kielelezo cha ustawi na maendeleo ya uchumi wa Tanzania na yanathibitisha moyo wa ujasiriamali na ubunifu wa Watanzania,kwa kuzileta pamoja biashara kutoka sekta mbalimbali, maonesho haya hayaoneshi uwezo wetu wa kiuchumi bali pia yanachochea ushirikiano wa pamoja unaowezesha ukuaji wa uchumi,”amesema.