Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
BENKI ya Biashara (TCB) imechangia mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya sh mil 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Goweko kilichoko Wilayani Uyui Mkoani hapa ili kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa kata hiyo.
Akikabidhi msaada huo jana kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Chichi Banda alisema wametoa mchango huo ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Alisema TCB imekuwa ikitoa mchango wa aina hiyo kila mwaka ili kutekeleza mpango wao wa kurejesha sehemu ya faida kwa wananchi ili kuboreshea utoaji huduma kwa jamii katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya.
Meneja aliongeza kuwa Benki hiyo ni mali ya Serikali hivyo msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za wananchi wa kata ya Goweko ili waweze kupata huduma za afya karibu zaidi.
Akipokea mssaada huo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ambaye ni diwani wa kata hiyo, Shaban Katalambula aliishukuru benki hiyo na kuahidi kutumia msaada huo kwa lengo lililokusudiwa.
Alisema kukamilika ujenzi wa kituo hicho kusaidia kuondoa kero ya wananchi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 80 kufuata huduma za upasuaji katika Kituo kingine.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Goweko Hamisi Banka aliishukuru TCB na kuomba Taasisi nyingine za kifedha kusaidia ujenzi wa zahanati na vituo vya afya ili kupunguza usumbufu wanaopata wananchi hususani akinamama wajawawazito.
Aliomba serikali iwasaidie ili kituo hicho kikamilike haraka na kuwekwa vifaa ili kuanza kutoa huduma.
Awali Meneja wa TCB Mkoa wa Tabora Timony Joseph alisema benki hiyo inawajali wananchi na itaendeelea kuunga mkono juhudi zao za kujiletea maendeleo ili kuimarisha na kuboresha huduma za kijamii.
Hadi sasa wakazi wa kata hiyo wameshachangia tofari 4,340 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hicho ambapo kitakapokamilika kitaweza kuhudumia wakazi wa kata hiyo na zile za jirani ikiwemo Nsololo na Kizengi.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa