November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCAA-CCC yaahidi huduma bora kwa wadau wa usafiri wa anga

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA-CCC) limesema litaendelea kuhakikisha ya kwamba watumiaji wa huduma za usafiri wa anga Tanzania wanapata huduma kwa wakati na kufurahia safari zao.

Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bw. Innocent Paul Kyara katika Salamu zake za Mwaka Mpya wa 2023.

“Kama kauli mbiu yetu inavyosema Haki zako, Maslahi yako ndiyo lengo letu, Mwaka 2023 tumejipanga zaidi kuendelea kuwawezesha na kuwawakilisha watumiaji kwa weledi wa hali ya juu na tunategemea huduma bora zaidi kama watumiaji wa huduma za usafiri wa anga Tanzania.” Alisisitiza Bw. Kyara.

Alisema katika mwaka 2022 sekta ya usafiri wa anga iliendelea kuboreka baada ya kupitia katika kipindi kigumu kutokana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Uviko 19 (Covid19). Ikumbukwe sekta ya usafiri wa anga ni miongoni mwa sekta zilizoathirika kwa kiasi kikubwa na ugojnwa huu.

Alisema kwa wakati huu ambao TCAA-CCC inaelekea mwishoni mwa mwaka 2022 na kuanza mwaka mpya 2023, ni wakati sahihi wa kufanya tathmini ya yale yaliyotokea katika mwaka unaoisha na kubaini maeneo ambayo taasisi ilifanya vizuri na maeneo ambayo palijitokeza changamoto kwa lengo la kuweka mikakati ya kuboresha katika mwaka ujao.

Katika mwaka huu tumeshuhudia kuongezeka kwa idadi ya watumiaji kwa maana ya abiria na mizigo bila kusahau miruko ya ndege hapa nchini kwetu kulinganisha na kipindi kilichopita,
Hatua hii inatokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali ikiwemo Kampeni iliyoendeshwa na Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuvutia watalii nchini kwetu kupitia filamu ya Royal Tour.

Jitihada nyingine zilizofanywa na Serikali ni kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali. Ikumbukwe Sekta ya usafiri wa anga ni sekta muhimu ya kuchochea ukuaji wa sekta nyingine.

Aidha, ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege unaohusisha njia za kurukia ndege na majengo ya abiria ni hatua zinazohitaji pongezi kubwa kwa Serikali. Tukichukulia mfano mmoja, kuanza kwa Ujenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Msalato Mkoani Dodoma, uwanja wa ndege ambao utaruhusu ndege kubwa zinazochukua abiria wengi kwa wakati mmoja kuweza kutua katika mkoa huu wa Dodoma, ambao ndio makao makuu ya Serikali na Nchi yetu.